Jan 19, 2022 10:23 UTC
  • Utawala ghasibu wa Kizayuni washadidisha kamatamata dhidi ya raia wa Palestina

Wazayuni maghasibu wamebomoa nyumba kadhaa za raia wa Palestina na kuwatia mbaroni Wapalestina 27 ikiwa ni katika kuendelea uadui na chuki za utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Klabu ya mateka wa Kipalestina imeripoti kuwa, Wazayuni maghasibu leo Jumatano wamewatia mbaroni Wapalestina 26 kutoka familia ya Salhiya baada ya kuvamia na kubomoa nyumba zao katika eneo la Sheikh Jarrah huko Baitul Muqaddas.  

Klabu hiyo jana pia ilitangaza kuwa, tangu kuanza mapambano ya al Naqab, utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu umewatia nguvuni karibu Wapalestina 150.  

Kwa mujibu wa ripot hiyo, Idadi kubwa ya raia wa Palestina waliokamatwa wameachiwa huru baada ya kushikiliwa kwa muda; huku baadhi yao pia wakiendelea kuhojiwa na utawala wa Kizayuni. Wanawake na watoto ni kati ya raia hao wa Palestina wanaoshikiliwa na Israel, huku Wapalestina wengine 69 wakiendelea kushikiliwa katika korokoro za utawala wa Kizayuni. 

Duru za ndani ya Palestina pia zimetangaza kuwa wanajeshi wa Kizayuni jana waliwatia nguvuni karibu wakazi 41 wa vijiji vya al Naqab ambao wengi wao ni watoto wadogo. Wazayuni wanaendeleza hujuma na mashambulizi yao kila siku katika maeneo mbalimbali ya Palestina kwa hatua zao za mabavu na kupenda kujitanua huku wakiwaua shahidi, kuwajeruhi na kuwatia mbaroni raia wa Palestina.

Israel yawatia mbaroni Wapalestina wa vijiji vya al Naqab 

Tags