Mazungumzo ya mapatano; mchakato wenye uhakika wa kufeli
(last modified Mon, 30 May 2016 04:21:30 GMT )
May 30, 2016 04:21 UTC
  • Mazungumzo ya mapatano; mchakato wenye uhakika wa kufeli

Katika muendelezo wa radiamali na hisia zinazoonyeshwa na fikra za wananchi pamoja na makundi ya muqawama ya Palestina kuhusiana na harakati zenye lengo la kufufua mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani na utawala wa Kizayuni, harakati ya Jihadul Islami ya Palestina, nayo pia imesisitiza kuwa mwisho wa mazungumzo hayo ni kugonga mwamba na kufeli tu.

Khalid al-Batash, kiongozi mwandamizi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema, hatua zozote zinazochukuliwa kuhusiana na mazungumzo ya mapatano baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni mwishowe zitafeli na kugonga mwamba tu.

Al-Batash ameyasema hayo huko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan katika maadhimisho ya kuwaenzi Wapalestina waliouawa shahidi katika Intifadha mpya ya Quds.

Amesema mazungumzo ya mapatano hayana faida yoyote kwa Wapalestina na kuongeza kuwa anawashauri viongozi na maafisa wa nchi za Kiarabu waachane na mazungumzo ya mapatano na kujiunga na muqawama wa Palestina.

Mazungumzo ya mapatano kati ya utawala wa Kizayuni na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa upatanishi wa Marekani yalivunjika mwezi Aprili mwaka 2014 kutokana na ukwamishaji wa utawala wa Kizayuni na hasa kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Hayo yamejiri katika hali ambayo, katika miezi ya karibuni, Ufaransa imeanzisha harakati mpya za kuyafufua mazungumzo ya mapatano, ambayo matokeo yake ni kikao kilichopangwa kufanyika tarehe 3 ya mwezi ujao wa Juni huko mjini Paris.

Duru mpya ya harakati za kufufua mazungumzo eti ya amani ya Mashariki ya Kati inaanzishwa ilhali utawala wa Kizayuni wa Israel umeukataa mpango huo.

Japokuwa mipango inayoitwa ya 'amani' ya Mashariki ya Kati ambayo imependekezwa hapo kabla na nchi za Magharibi zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni au na nchi za Kiarabu zinazounga mkono mapatano inatayarishwa kukidhi na kulinda maslahi ya Israel, lakini utawala huo umekuwa na kawaida ya kuikataa mipango hiyo au kutoiheshimu na kukwamisha utekelezaji wake.

Ni muhimu kufahamu kwamba mpango wa 'amani' wa Ufaransa una vipengee kadhaa vinavyokidhi maslahi ya utawala wa Kizayuni na kuzidi kupoka haki za Wapalestina ikiwemo kuutambua utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa dola la Kiyahudi, kufutwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea makwao kwa kuwalipa fidia na kuwapatia makazi katika maeneo waliko hivi sasa pamoja na kuwapokonya silaha wanamapambano wa muqawama wa Palestina.

Mchakato wa mapatano wa njama ya madola ya Magharibi kuhusiana na kadhia ya Palestina umeandaliwa kwa namna inayoudhaminia utawala wa Kizayuni kuendeleza ziasa zake za kujipanua kwa kisingizio cha suluhu na amani. Pamoja na hayo utendaji wa utawala wa Kizayuni unaonesha kuwa utawala huo ghasibu hautosheki na upendeleo huo wa madola ya Magharibi, bali unachotaka hasa ni kujipatia fursa zote na kufuta kikamilifu haki zote za Wapalestina.

Kushadidisha vitendo vya ukatili na ukandamizaji kunakofanywa na utawala wa Kizayuni hakujabakisha chembe yoyote ya shaka kuwa utawala huo ni mpinzani wa suluhu na amani na kwamba hatua zozote za kutaka kufikia amani na mapatano na Israel haziwezi kuwa na tija yoyote.

Ukweli ni kwamba, kutokana na sura halisi ya hila na njama iliyonayo mipango ya mazungumzo ya mapatano, sio tu imekuwa na taathira hasi kwa Wapalestina lakini kutokana na kasoro chungu nzima ilizonazo haijaweza katu kuwa na uwezo wa kujitosheleza kutatua kiadilifu mgogoro wa Palestina; na kukwama na kuvunjika kila mara mazungumzo hayo kumezidi kuweka wazi udhaifu wa mchakato wa mapatano katika kutatua mgogoro huo.../