Kuwait yataka Israel ifukuzwe katika Umoja wa Mabunge Duniani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81576-kuwait_yataka_israel_ifukuzwe_katika_umoja_wa_mabunge_duniani
Spika wa Bunge la Kuwait amekosoa sera za undukumakuwili za Jamii ya Kimataifa kuhusu utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kutaka ujumbe wa utawala huo utimuliwe katika kikao cha Umoja wa Kimataifa wa Mabunge.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Mar 20, 2022 03:52 UTC
  • Kuwait yataka Israel ifukuzwe katika Umoja wa Mabunge Duniani

Spika wa Bunge la Kuwait amekosoa sera za undukumakuwili za Jamii ya Kimataifa kuhusu utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kutaka ujumbe wa utawala huo utimuliwe katika kikao cha Umoja wa Kimataifa wa Mabunge.

Akihutubia kikao cha uratibu cha nchi za Kiarabu wanachama wa Umoja wa Mabunge Duniani kilichofanyika jana nchini Indonesia, Marzouk al Ghanim, amekosoa sera za undumakuwili za jamii ya kimataifa na akasisitiza kwa kusema: "kimsingi, sisi tunalaani aina yoyote ile ya uvamizi, kwa sababu miaka 30 nyuma nchi yetu pia ilivamiwa na kukaliwa, kwa hivyo tunapinga kila aina ya uvamizi."

Al Ghanim ameongezea kwa kuhoji: "vipi itakiwe kufukuzwa ujumbe wa Russia kwa sababu ya vita vilivyoanza siku kadhaa tu nyuma, lakini ujumbe wa Israel haufukuzwi, wakati utawala huo wa Kizayuni umeivamia na kuikalia kwa mabavu Palestina kwa zaidi ya miaka 60?"

Marzouk al Ghanim

Kinyume na baadhi ya watawala wafanya mapatano wa nchi za Kiarabu, Kuwait inafuata sera ya kupinga uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Viongozi wa nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi kila mara wamekuwa wakionyesha msimamo wa kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na kupinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Kizayuni.

Na kwa sababu hiyohiyo pia, tarehe 7 Aprili wizara ya habari ya Kuwait ilizuia rasmi kuonyeshwa nchini humo filamu ya sinema iitwayo Kifo Kwenye Nile (Death on the Nile) kwa sababu nyota mwanamke wa filamu hiyo ni askari wa zamani wa jeshi la utawala haramu wa Israel.

Halikadhalika, mapema mwezi huu, wasomi wa vyuo vikuu vya Kuwait walitangaza kususia kongamano lililokuwa limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Bahrain baada ya kubainika kuwa ujumbe kutoka utawala haramu Israel umealikwa kushiriki kongamano hilo.

Mnamo mwezi Februari mwaka huuhuu pia, Muhammad Al Awadi  Mchezaji maarufu wa mchezo wa tenisi kutoka Kuwait alikataa kupambana na mcheza tenisi wa utawala wa Kizayuni, katika mashindano ya J4 Dubai yaliyofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), hatua ambayo ilisifiwa na kupongezwa na wanaharakati wengi wa kijamii.../