Mamlaka ya Ndani yaitaka Uingereza iitambuliwe rasmi Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82256-mamlaka_ya_ndani_yaitaka_uingereza_iitambuliwe_rasmi_palestina
Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametoa wito kwa serikali ya Uingereza kutekeleza uamuzi wa Baraza la Wawakilishi wa kuitambua Palestina.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Apr 07, 2022 22:16 UTC
  • Mohammad Ibrahim Shtayyeh
    Mohammad Ibrahim Shtayyeh

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametoa wito kwa serikali ya Uingereza kutekeleza uamuzi wa Baraza la Wawakilishi wa kuitambua Palestina.

Katika mazungumzo yake ya jana Alhamisi huko Ramallah na wajumbe 15 wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha Conservative, Mohammad Ibrahim Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, kwa mara nyingine tena ameitaka Uingereza itekeleze majukumu yake ya kisiasa na kihistoria kwa kuitambua rasmi Palestina.

Vilevile ameitaka Uingereza kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni wa Israel ili uruhusu kufanyika uchaguzi katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu (Jerusalem) kwa misingi ya makubaliano yaliyotiwa saini baina ya pande mbili.

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu, Israel ni utawala wa kibaguzi wa apartheid na amesisitiza udharura wa kutekelezwa sheria za kimataifa na kuuwajibisha utawala wa Kizayuni kutokana na hatua zake za kukiuka haki za wananchi wa Palestina.

Mohammad Ibrahim Shtayyeh 

Miaka mingi iliyopita chama cha Labour (kambi ya upinzani nchini Uingereza) kiliunga mkono kuundwa kwa taifa huru la Palestina.

Ijapokuwa imepita zaidi ya miaka 70 tangu kutangazwa kuwepo utawala wa Kizayuni wa Israel hapo Mei 14, 1948 baada ya kuvamiwa na kutwaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina, mizozo na migogoro katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu bado inaendelea, na Wapalestina daima wamekuwa wakitangaza kuwa wataendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao hadi pumzi yao ya mwisho.