Iran yasema Wapalestina wana haki ya kupambana na Israel
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Wapalestina wana haki ya kisheria na iliyo wazi ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia ardhi zao kwa mabavu.
Katika taarifa siku ya Jumamosi, Saeed Khatibzadeh amesema mapamabano ya Wapalestina ni jibu kwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo matakatifu katika mji wa Quds na jinai zinginezo za utawala huo dhidi ya Wapalestina.
Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono harakati za Wapalestina za kukomboa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akiashiria matukio ya hivi karibuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, Khatibzadeh amesema ubaguzi, ukandamizaji, umwagaji damu, kuwekwa kizuizini, udhalilishaji pamoja na ugaidi wa wazi ni kati ya hatua zinazochukuliwa na utawala wa kibaguzi wa Israel na vitendo hivyo ni chanzo cha mgogoro katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Kauli hiyo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekuja baada ya ufyatuaji risasi Tel Aviv ambapo watu wasiopungua wawili wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa.
Shambulizi hilo la ulipizaji kisasi limetekelezwa na kijana Mpalestina aliyetambuliwa kama Ra'ad Fathi Hazem.
Harakati kadhaa za kupigania ukombozi wa Palestina na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon zimepongeza oparesheni hiyo na kuitaja kuwa ya kishujaa.