UAE, Bahrain na Saudia zinahasimiana na kila anayepinga Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82720-uae_bahrain_na_saudia_zinahasimiana_na_kila_anayepinga_israel
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen anasema Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Saudi Arabia zinahasimiana na kila ambaye ni adui wa utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa madola hayo matatu hayataki uthabiti wa Waislamu duniani na daima yanatekeleza njama chafu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2022 06:34 UTC
  • UAE, Bahrain na Saudia zinahasimiana na kila anayepinga Israel

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen anasema Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Saudi Arabia zinahasimiana na kila ambaye ni adui wa utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa madola hayo matatu hayataki uthabiti wa Waislamu duniani na daima yanatekeleza njama chafu.

Akizungumza Jumanne akiwa Sana'a, Kiongozi wa Ansarullah Abdul-Malik Badruldeen al-Houthi amesema: "Utawala wa Al Khalifa wa Bahrain, utawala wa UAE wa Aal Nahyan pamoja na utawala wa Aal Saud zimeanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa jina la usalama na uthabiti bandia katika eneo." Amesema tawala hizo ziko radhi kutumikia Marekani na Israel na kuongeza tawala hizo tatu za Kiarabu ni za kidhalimu na zinachochea fitina katika ulimwengu wa kisiasa kwa kutumia pesa, propaganda za vyombo vya habari na ushawishi wa kisiasa.

Ameongeza kuwa UAE, Bahrain na Saudia zinachukizwa na kila ambaye anahasimiana na Israel likiwemo taifa la Yemen. Amesema tawala hizo za Kiarabu zimeanzisha uhusiano na utawala wa Israel huku zikiwataja Wapalestina wanaopigania ukombozi wao kuwa ni magaidi.

Kiongozi wa Ansarullah aidha amesema wimbi jpya la hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ni ishara ya uhasama wa utawala huo dhidi ya Uislamu na matukufu yake.

Mrithi wa Ufalme wa Saudia Muhammad Bin Salman amekuwa akijikurubisha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

Ameongeza kuwa iwapo nchi za Kiislamu zitaungana na kuwa kitu kimoja, maadui watapoteza matumaini na watalazimika kulegeza masimamo.

Saudi Arabia huku ikiungwa mkono kwa hali na mali na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani, utawala wa Kizayuni, Uingereza na nchi kadhaa nyingine kama vile Sudan, mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha mashambulizi ya kijeshi ya pande zote dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu nchi hiyo maskini ya Kiarabu. 

Hadi sasa Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameshauawa katika vita hivyo vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, huku makumi ya maelfu wakijeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.