Wavamizi wavunja makubaliano ya Yemen, wazuia ndege kutua Sana'a
Naibu wa Mkuu wa Shirika la Ndege la Yemen amesema kuwa, madola vamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia yanazuia ndege kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Sana'a na huo ni uvunjaji wa wazi kabisa wa usimamishaji vita uliotangazwa na Umoja wa Mataifa.
Usimamishaji vita nchini Yemen ulianza kutekelezwa tarehe pili mwezi huu wa Aprili kwa pendekezo la Umoja wa Mataifa lakini muda wote muungano vamizi hauheshimu usitishaji vita huo. Muungano vamizi unaoongozwa na Saudia unaendelea kuuzingira Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a na vile vile hadi sasa umeshazuia meli kadhaa za mafuta za Yemen.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya SABA, Raid Talib Jabal, Naibu wa Mkuu wa Shirika la Ndege la Yemen amesema, nchi vamizi zimekataa kutoa idhini kwa shirika hilo kutumia ndege zake kama ambavyo leo Jumapili zimezuia kutua ndege ambazo zilikuwa zimepangwa kuingia kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a. Amesisitiza kuwa, kitendo hicho cha nchi vamizi ni kutoheshimu waziwazi usimamishaji vita uliotangazwa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa.
Katikati ya mwezi huu pia, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye makao makuu yake mjini Sana'a, alitaka kukomeshwa ukiukaji wa usitishaji vita huko Yemen unaofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia. Muhammad Abdulsalam aliwasilisha ombi hilo katika mazungumzo yake na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen.
Hadi katikati ya mwezi huu wa Aprili, muungano vamizi wa Saudia na Imarati ulikuwa umeshakiuka mara 1,647 usitishaji vita uliofikiwa huko Yemen tena katika kipindi cha wiki moja na kidogo tu tangu kufikiwa mapatano hayo tarehe ya Pili mwezi huu wa Aprili sasa moja usiku kwa wakati wa Yemen.