Hashdu Shaabi yashambulia maficho ya magaidi Iraq; yaua kadhaa miongoni mwao
(last modified Tue, 07 Jun 2022 08:03:57 GMT )
Jun 07, 2022 08:03 UTC
  • Hashdu Shaabi yashambulia maficho ya magaidi Iraq; yaua kadhaa miongoni mwao

Wanamapambano wa harakati ya wanamuqawa ya Hashdu Shaabi ya Iraq wameshambulia ngome na maficho ya mabaki ya wanachama wa magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi ajinabi kaskazini mwa Baghdad, mji mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Shirika la habari la Sabereen limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, magaidi zaidi ya 12 wameangamizwa katika operesheni hiyo, iliyofanyika katika mji wa Tarmiyah, mkoani Salahuddin. 

Kanali ya habari ya mtandao wa Telegram wenye mfungamano na harakati hiyo ya muqawama imeripoti kuwa, operesheni hiyo ya mashambulizi ilifanywa jana Jumatatu na Brigedi ya 12 ya harakati ya Hashdu Shaabi.

Haya yanajiri siku moja baada ya Kitengo cha Taifa cha Intelijensia ya Iraq (INIS) kutangaza kuwa, kimewatiwa mbaroni watu 14 waliokuwa wakila njama za kufanya operesheni ya mashambulizi makubwa mjini Baghdad.

Wanaharakati wa Hashd Shaabi wakiwa kwenye operesheni

Katika miezi ya karibuni, mashambulio ya wanachama wenye mfungamano na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) yameshamiri katika sehemu za mashariki na kaskazini ya Iraq.

Wananchi wengi na makundi mbalimbali ya nchi hiyo wanaamini kuwa, kuongezeka kwa harakati za Daesh ni matokeo ya njama ya Marekani nchini Iraq inayolitumia suala hilo ili iweze kubaki na kuendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo.