Magaidi wameua kwa siku moja raia 270 nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8545-magaidi_wameua_kwa_siku_moja_raia_270_nchini_syria
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa raia wasiopungua 270 wameuliwa katika mashambulio yaliyofanywa na magaidi nchini Syria katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2016 23:31 UTC
  • Magaidi wameua kwa siku moja raia 270 nchini Syria

Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa raia wasiopungua 270 wameuliwa katika mashambulio yaliyofanywa na magaidi nchini Syria katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imeeleza kuwa kundi la kigaidi la Jabhatun-Nusra lenye mfungamano na Al-Qaeda nchini Syria limepata wapiganaji wapya na hivyo limeanzisha wimbi jipya la vita.

Ripoti zinaeleza kuwa wanachama wa Jabhatun-Nusra wamejiimarisha tena katika maeneo wanayoyashikilia kwa pamoja na waasi wanaojiita "wapinzani wenye misimamo ya wastani".

Siku ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov alitangaza kuwa Marekani imeitaka Moscow iache kufanya mashambulio ya anga kwenye ngome za Jabhatun-Nusra kwa sababu inahofiwa mashambulio hayo yatawalenga waasi wanaojiita "wapinzani wenye misimamo ya wastani".

Awali Russia ilikuwa imetoa pendekezo kwa Marekani la kufanya operesheni za pamoja za mashambulio ya anga dhidi ya kundi la kigaidi la Jabhatun-Nusra na makundi mengine ya kigaidi yaliyokiuka makubaliano ya usitishaji vita nchini Syria, lakini Washington ilipinga pendekezo hilo.

Vita na machafuko ya miaka mitano nchini Syria hadi sasa yameua watu wapatao 470,000, yamejeruhi watu zaidi ya milioni 1.9 na kuwafanya mamilioni ya wengine wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.../