UN: Jela za siri za Imarati nchini Yemen zinatumiwa kutesa mahabusu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i86458-un_jela_za_siri_za_imarati_nchini_yemen_zinatumiwa_kutesa_mahabusu
Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ghasia na mateso katika jela za siri za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) huko Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2022 23:06 UTC
  • UN: Jela za siri za Imarati nchini Yemen zinatumiwa kutesa mahabusu

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ghasia na mateso katika jela za siri za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) huko Yemen.

Kamisheni Kuu ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema mateso na unyanyasaji unaofanywa na vikosi vya jeshi la UAE, idara za usalama za serikali na makundi yasiyo ya kiserikali yenye silaha nchini Yemen, unatia wasiwasi.

Kamisheni hiyo imeashiria ushiriki wa Umoja wa Falme za Kiarabu katika mapigano ya Yemen na kutoa wito wa kuanzishwa mchakato wa kufuatilia uhalifu na jinai za mateso na ukati huo na kuhakikisha waathiriwa wanatendewa haki na uadilifu. 

Kamishna wa Haki za Kibinadamu wa UN pia ametoa wito kwa serikali ya UAE kuongeza juhudi za kukomesha unyanyasaji wa kijamii na vitendo vingine vyenye madhara kwa kupitisha sheria mpya na kuandaa kampeni za uzinduzi.

Gazeti la Le Monde linalochapishwa nchini Ufaransa limefichua kuwa, Imarati ina jela zisizopungua 18 za siri ndani ya ardhi ya Yemen.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Umoja wa Falme za Kiarabu una jela zisizopungua 18 ndani ya ardhi ya Yemen; na askari wa vikosi vya Marekani ndio wanaofanya kazi ya kuwasaili wafungwa wanaoshikiliwa ndani ya jela hizo.

Le Monde limebainisha kuwa, moja ya jela hizo za siri za Imarati iko kwenye taasisi moja ya gesi ya shirika la mafuta la Total la Ufaransa kusini mwa Yemen.

Tangu Machi 2015 na kwa misaada na uungaji mkono wa Marekani, Saudia na Imarati zimeivamia kijeshi Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa angani, nchi kavu na baharini. Uvamizi na hujuma za kijeshi za Saudia na waitifaki wake, hadi sasa zimeshaua zaidi ya watu elfu 16, kujeruhi makumi ya melfu na kuwafanya mamilioni ya watu wapoteze makazi yao na kuwa wakimbizi.