Uturuki kushirikiana na Syria dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Marekani
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema kuwa nchi yake iko tayari kusaidia serikali ya Syria katika juhudi zake za kuwafurusha wanachama wa kundi la wanamgambo wa Kikurdi (YPG) wanaoungwa mkono na Marekani kutoka maeneo yenye utajiri wa nishati kaskazini mashariki mwa Syria.
Cavusoglu amekiambia kituo cha habari cha TV1000 cha lugha ya Kituruki kwamba taifa lake liko tayari kushirikiana na Damascus katika kampeni hiyo.
Mwanadiplomasia mkuu wa Uturuki amesema,"Tutatoa kila aina ya uungaji mkono wa kisiasa kwa kazi ya utawala [wa Syria] katika suala hili. Ni haki ya asili kabisa ya serikali kufuta shirika la kigaidi katika eneo lake."
Matamshi ya Cavusoglu yanakuja huku kukiwa na vitisho vya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kuhusu uwezekano wa operesheni mpya ya kijeshi kaskazini mwa Syria.
Mapema mwezi huu, Erdogan alisema mpango wa Uturuki wa mashambulizi mapya ya kijeshi kaskazini mashariki mwa Syria dhidi ya wanachama wa YPG utasalia kwenye ajenda hadi masuala ya usalama yatakaposhughulikiwa.
Mnamo Julai 19, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatollah Seyed Ali Khamenei alimwambia Erdogan aliyekuwa safarini chini hapa kwamba mashambulizi yoyote ya Uturuki dhidi ya Syria yatakuwa na "madhara" kwa Syria, Uturuki yenyewe na eneo zima. Aidha Kiongozi Muadhamu alitaka suala hilo litatuliwe kwa njia ya mazungumzo kati ya Syria, Uturuki, Iran na Russia.
Russia pia hapo awali iliitaka Ankara "kujizuia" na shambulio. Erdogan mnamo Mei 23 aliashiria operesheni mpya ya mpaka wa Uturuki kaskazini mwa Syria kwa lengo lililotangazwa la kuunda eneo salama la upana wa kilomita 30 (maili 18.6) kwenye mpaka wa Uturuki na Syria.
Ankara inalitambua kundi la YPG kama kundi la kigaidi linalofungamana na chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK), ambacho kimekuwa kikitaka kujitenga eneo la Wakurdi nchini Uturuki tangu 1984.
Rais wa Syria Bashar al-Assad na maafisa wengine wakuu wamesema Damascus itajibu kupitia njia zote halali mashambulizi ya ardhini yanayoendelea Uturuki.