IGAD: Pembe ya Afrika kukosa mvua kwa mwaka wa tano mtawalia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i87578-igad_pembe_ya_afrika_kukosa_mvua_kwa_mwaka_wa_tano_mtawalia
Ukame wa kutisha unaolikumba eneo la Pembe ya Afrika ni mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40, huenda ukawa mbaya zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2022 22:02 UTC
  • IGAD: Pembe ya Afrika kukosa mvua kwa mwaka wa tano mtawalia

Ukame wa kutisha unaolikumba eneo la Pembe ya Afrika ni mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40, huenda ukawa mbaya zaidi.

Hiyo ni kulingana na tathmini kutoka kituo cha utabiri wa hali ya hewa cha kikanda cha Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Mashariki mwa Afrika (IGAD)

Msimu wa mvua ambao huanza mwezi Oktoba hadi mwezi Desemba ni muhimu sana kwa Pembe ya Afrika. Kwa kawaida huleta hadi 70% ya mvua kwa mwaka katika baadhi ya maeneo, kwa mfano mashariki mwa Kenya. Lakini utabiri ni mbaya tena: mvua zitachelewa na zitanyesha kwa kiwango kidogo, imeeleza taarifa ya tathmini hiyo.

Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yanahofia athari za msimu huu wa tano wa mvua kukosa katika uzalishaji wa kilimo na mifugo, wakati uhaba wa chakula tayari unafikia viwango vya kutisha.

Baa la njaa linatishia maisha ya mamilioni ya watu katika eneo la Pembe ya Afrika

 

Ripoti mbalimbali za mashirika ya utoaji misaada zinaonyesha kuwa, eneo la Pembe ya Afrika lingali linakabiliwa na hatari ya baa la njaa huku katika baadhi ya maeneo hali ikiwa ni mbaya sana.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, katika eneo la Pembe ya Afrika hali ya ukame inazidi kutishia uwezekano wa baa la njaa kwenye eneo hilo linalojumuisha Kenya, Somalia na Ethiopia huku Umoja wa Mataifa ukisema takribani watu milioni 18.4 huamka kila siku bila uhakika wa mlo huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia milioni 20 mwezi ujao wa Septemba.