Waziri Mkuu wa Iraq kujiuzulu iwapo mkwamo wa kisiasa utaendelea kushuhudiwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i87634-waziri_mkuu_wa_iraq_kujiuzulu_iwapo_mkwamo_wa_kisiasa_utaendelea_kushuhudiwa
Waziri Mkuu wa Iraq ametishia kuwa atajiuzulu wadhifa wake huo iwapo mkwamo na mgogoro wa kisiasa utaendelea kushuhudiwa nchini huo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 31, 2022 07:22 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq kujiuzulu iwapo mkwamo wa kisiasa utaendelea kushuhudiwa

Waziri Mkuu wa Iraq ametishia kuwa atajiuzulu wadhifa wake huo iwapo mkwamo na mgogoro wa kisiasa utaendelea kushuhudiwa nchini huo.

Mustafa al-Kadhimi alitoa indhari hiyo jana Jumanne na kusisitiza kuwa, "Nitaachia ngazi kulalamikia hali ya kisiasa isiyoeleweka."

Taifa hilo la Kiarabu limekuwa katika mvutano wa kisiasa, uliopelekea kushindwa kuunda serikali tangu baada ya uchaguzi wa Bunge wa Oktoba mwaka jana.

Kadhimi amebainisha kuwa, kamisheni ya uchunguzi imeundwa ili kufuatilia chimbuko la silaha zilizotumika katika machafuko ya kisiasa yaliyoshuhudiwa tangu Jumatatu.

Kwa akali watu 30 wameuawa, huku mamia ya wengine wakijeruhiwa katika ghasia za siku mbili mjini Baghdad.

Kiongozi mashuhuhuri wa kidini Iraq, Muqtada Sadr

Hapo jana, kiongozi mashuhuhuri wa kidini, Muqtada Sadr aliwataka wafuasi wake waache vurugu na fujo, mbali na kuliomba radhi taifa. Juzi Jumatatu, Sard alitangaza kujiuzulu siasa, hatua iliyoibua hasira miongoni mwa wafuasi wake, ambao walianza kufanya maandamano ya ghasia, na kuvamia ofisi za serikali.

Waziri Mkuu wa Iraq amekaribisha tangazo hilo la Muqtada Sadr na kusisitiza kuwa, mwito wa mwanachuoni huo wa kutaka kukomeshwa vitendo vya ghasia ni wa kizalendo, na kwamba wakati umefika wa kutoa kipaumbele kwa mazungumzo ili kujaribu kutatua mkwamo wa kisiasa uliopo.