Wazayuni wazidisha jinai, waua shahidi makumi ya Wapalestina katika mwezi mmoja
Takwimu zilizotolewa na vyombo vya habari vya Palestina zinaonesha kuwa utawala wa Kizayuni umeshadidisha jinai zake dhidi ya wananchi wasio na hatia kiasi kwamba katika mwezi mmoja tu ulioisha wa Agosti, Israel imeua shahidi Wapalestina 59 katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Tovuti ya Arab24 imeripoti kuwa, tangu mwanzo mwa mwaka huu wa 2022 hadi kabla ya mwezi ulioisha wa Agosti, utawala katili wa Kizayuni ulikuwa umeshaua shahidi Wapalestina 143. Pamoja na kwamba hiyo si idadi ndogo ya Wapalestina wanaouliwa kidhulma, kiholela na kila siku na utawala wa Kizayuni, lakini mauaji ya mwezi ulioisha wa Agosti ni makubwa kiasi kwamba ni sawa na asilimia 41 ya mauaji yote yaliyofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina zinaonesha kuwa, ndege za kijeshi za Israel ziliua shahidi Wapalestina 50 katika vita vya siku tatu vya Ukada wa Ghaza. Kati ya Wapalestina hao waliouliwa kikatili na utawala wa Kizayuni, 16 walikuwa na umri wa chini ya miaka 18.
Utawala huo dhalimu uliua shahidi pia Wapalestina 9 katika Ukingo wa Magharibi wa Jordan ndani ya mwezi huo wa Agosti. Watano kati yao waliuawa huko Nablos na walioubakia waliuliwa kikatili katika kambi za wakimbizi za Jenin, al Khalil, Quds inayokaliwa kwa mabavu na Tubas.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, mji wa Nablos ndio uliokuwa uwanja mkubwa zaidi wa muqawama wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan mwezi uliopita. Hii ni katika hali ambayo, kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Jenin ndiyo iliyokuwa kitovu cha muqawama wa Wapalestina huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika miezi ya kabla ya Agosti.