Udharura wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i87832-udharura_wa_kufanyika_mazungumzo_ya_kitaifa_nchini_iraq
Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq kwa mara nyingine ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2022 21:43 UTC
  • Udharura wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa nchini Iraq

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq kwa mara nyingine ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi hiyo.

Matukio ya miezi 10 iliyopita nchini Iraq yanaweza kugawanywa katika hatua mbili tofauti. Hatua ya kwanza ni kuanzia kufanyika uchaguzi mkuu wa bunge hadi wakati wa kujiuzulu Harakati ya Sadr mwezi Juni na tangu wakati huo hadi sasa. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2021, mashauriano ya kisiasa kuhusu mpangilio wa madaraka ya Iraq yalianza, lakini tabia ya Muqtada Sadr na nia yake ya kutaka kuwa mtu wa kwanza kisiasa nchini humo ilivuruga kabisa mashauriano hayo.

Ukaidi wa kisiasa wa harakati ya Sadr hatimaye ulisababisha mkwamo katika kuarifishwa rais na waziri mkuu mpya wa Iraq, ambapo Sadr hatimaye aliwataka wawakilishi wa kundi lake wajiondoe bungeni na hivyo kuielekeza Iraq kwenye njia ya mvutano na kufungwa milango yote ya mazungumzo.

Mustafa al-Kadhimi

Tangu harakati ya Sadr ijiondoe bungeni mwezi Juni uliopita, taasisi za utawala za Iraq zimekuwa zikilengwa na ghasia za mitaani, na kwa mara nyingine tena, machafuko na tabia ya kutumia mabavu imekuwa ikitawala anga ya mazungumzo na ustaarabu wa kiraia. Mapigano ya umwagaji damu baada ya kipindi cha ugaidi wa Daesh, yalifikia kilele Jumatatu ya tarehe 29 Agosti huko Iraq ambapo watu 30 walipoteza maisha na wengine wasiopungua 700 kujeruhiwa.

Sasa Waziri Mkuu wa Iraq kwa mara nyingine tena anasisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kama njia ya kujinasua kwenye mkwamo wa kisiasa uliopo, wakati ambao tangu huko nyuma Mfumo wa Uratibu wa Kishia umekuwa ukisisitiza mara kwa mara kwamba mazungumzo ya kitaifa ndiyo njia pekee ya kujikwamua kwenye mkwamo wa kisiasa uliopo hivi sasa nchini.

Hata hivyo, vuguvugu la Sadr hadi sasa limekuwa likikataa kushiriki mazungumzo yoyote ya iana hiyo. Katikati ya mwezi uliopita wa Agosti, al-Kadhimi aliitaka mirengo yote ya kisiasa ya Iraq kushiriki katika mazungumzo muhimu ya kisiasa huko Baghdad ili kujaribu kutatua mzozo huo wa kisiasa, mazungumzo ambayo yalifanyika, lakini vuguvugu la Sadr likakataa kushiriki na badala yake likawachochea wafuasi wake wamiminike na kukusanyika katika eneo la kijani kibichi mjini Baghdad ili kukwamisha mambo na kuvuruga usalama wa eneo hilo ambalo lina taasisi muhimu za serikali.

Bisla shaka mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuondoa mkwamo wa kisiasa unaoshuhudiwa huko Iraq. Pamoja na hayo ni wazi kuwa suala hilo linapasa kuzingatiwa kwa dhati na kwa nia njema na pande zote za kisiasa ambapo wanasiasa wanapasa kuachana na kutoa nara tupu zisizo na maana na kujihusisha vilivyo na jitihada zozote zenye lengo la kutatua mzozo huo. Makundi yote ya kisiasa na yenye ushawishi mkubwa Iraq yanapasa kushiriki kwenye mazungumzo hayo ya kitaifa na iwapo kundi lolote litakataa kushiriki basi makundi mengine yaliyoshiriki yachukue uamuzi wa kutekeleza masuala yaliyopitishwa bila kusita.

Wafuasi wa Muqtada Sadr wakiwa wameyavamia majengo ya bunge mhini Baghdad

Jambo jingine muhimu ni kwamba makundi ya Iraq yanapaswa kuketi kwenye meza ya mazungumzo bila kutanguliza masharti yoyote, kwa sababu masharti kama hayo yanaweza kuvuruga mchakato mzima wa mazungumzo. Wakati huo huo, ajenda ya mazungumzo inapaswa kuwekwa wazi.

Hii leo Iraq inakabiliwa na msururu wa mivutano na tofauti ambazo iwapo hazitatatuliwa kwa njia muwafaka, hakutakuwepo na uwezekano wa kuondoa mkwamo wa kisiasa uliopo. Ukubwa wa masuala hayo bila shaka si hitajio la Iraq kwa sasa na wala hautaisaidia nchi hiyo kukabiliana na changamoto zilizopo.