Kukiri jeshi la Israel kwamba, lilimuua Shireen Abu Akleh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i87894-kukiri_jeshi_la_israel_kwamba_lilimuua_shireen_abu_akleh
Jeshi la utawala haramu wa Israel limekiri kwamba, Shireen Abu Akleh, mwanahabari wa Kipalestina wa Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na mmoja wa wanajeshi wa utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2022 03:59 UTC
  • Kukiri jeshi la Israel kwamba, lilimuua Shireen Abu Akleh

Jeshi la utawala haramu wa Israel limekiri kwamba, Shireen Abu Akleh, mwanahabari wa Kipalestina wa Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na mmoja wa wanajeshi wa utawala huo.

Shireen Abu Akleh aliyekuwa na umri wa miaka 51, ripota wa televisheni ya al-Jazeera yenye makao yake nchini Qatar, aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel tarehe 11 mwezi Mei mwaka huu wakati akiripoti uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina. 

Awali utawala ghasibu wa Israel ulikana kabisa kufanya mauaji hayo, lakini hivi sasa umejitokezaa na kukiri hadharani kwamba, jinai hiyo ilitekelezwa na mmoja wa wanajeshi wake.

Nukta muhimu kuhusiana na kadhia hii ni kwamba, uchunguzi kuhusiana na mauaji ya Shireen Abu Akleh umefanywa na jeshi la Israel lenyewe, katika hali ambayo jinai hii nayo imetekelezwa na mwanajeshi wa utawala huo haramu. Hii ni katika hali ambayo, mhalifu hawezi kuwa ndiye mtoa hukumu.  Ni kwa kuzingatia ukweli  huo ndio maana jeshi la Israel limedai katika taarifa yakke kwamba, mauaji hayo yalifanyika kimakosa.

 

Endapo uchunguzi wa mauaji hayo ungefanywa na kamati ya huru na ya kimataifa, matokeo yake yangeweza kuwa tofauti, na hata yumkini ingethibitishwa kwamba, yalitekelezwa kwa makusudi.

Madai ya Israel kwamba, mauaji hayo hayakufanywa kwa makusudi yametolewa pia kabla ya hapo na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani. Mwezi Julai mwaka huu, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilidai katika ripoti iliyolenga kuiondolea mashtaka Tel Aviv kwamba "Shireen Abu Akleh huenda aliuawa bila kukusudia kwa risasi iliyotoka upande wa wanajeshi wa Israel."

Kwa kuzingatia historia ya utawala huo haramu madai hayo hayana ukweli wowote na zaidi yanalenga kukwepa kutoa majibu na kuwajibishwa kufuatia jinai hiyo ya wazi.

Wajuzi wa mambo na waandishi wa habari wanaamini kuwa, madai ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, mauaji hayo yalifanyika kwa bahati mbaya ni kutaka kufunika kuwajibishwa Israel kwa kutenda jinai hiyo dhidi ya mwanahabari mkongwe Shireen Abu Akleh.

Kamati ya Kuwalinda Wanahabari imetangaza kuwa, taarifa ya jeshi la Israel imechelewa kutolewa, ni pungufu na haijatoa majibu wa kuwajibika.

Fauka ya hapo, sisitizo la kutokuwa ni ya makusudi mauaji dhidi ya ripota shahidi Shireen Abu Akleh linalenga kuzizuia Qatar na Palestina kufuatilia kadhia hiyo kisheria. Shireen Abu Akleh alikuwa ripota wa Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar lakini Mpalestina. Kwa msingi huo, nchi zote mbili Qatar na Palestina zinaweza kufuatilia kisheria mauaji mwanahabari huyo mahiri. Kabla ya hapo, Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar ilitangaza kuwa, imeunda kamati ya kimataifa ya kisheria kwa kuandaa faili la mauaji ya Shireen Abu Akleh na kulipeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Maandamano ya kulalamikia mauaji ya Shahidi Shireen Abu Akleh

 

Kuwauwa waandishi wa habari ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kunahesabiwa kuwa ni kuhujumu uhuru wa kusema na uhuru wa vyombo vya habari. Pamoja na sheria kukemea na kulaani hilo, lakini utawala ghasibu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu umekuwa ukitenda jinai kama hizi kwa wepesi na urahisi kabisa tena bila ya wasiwasi wowote. Himaya na uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi kwa utawala haramu wa Israel bila kusahau kigugumizi cha Umoja wa Mataifa na kutochukua kwake hatua za maana za kukabiliana na jinai hizo, ni mambo ambayo kwa hakika yameupa kichwa na kiburi utawala huo cha kuendelea kutenda mauaji na jinai kila leo dhidi ya Wapalestina. Kuanzia mwaka 2000 hadi sasa kwa akali waandishi habari 45 wameuawa na utawala wa Kizayunui wa Israel na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kimataifa kwa ajili ya kuupandisha kizimbani na kuuadhibu utawala huo ghasibu.

Kimya hicho kinaendelea katika hali ambayo, mauaji dhidi ya waandishi wa habari ni misdaqi na mfano wa wazi wa jinai za kivita. Israel imekuwa ikikariri mauaji na jinai hizo ili kuwazuia waandishi habari kufichua na kuwawekea wazi walimwengu jinai zinazofanywa na utawala huo katili dhidi ya Wapalestina.

Hapana shaka kuwa, kutochukuliwa hatua zozote za maana mkalaba na jinai za Israel ni jambo ambalo linayafanya mauaji na jinai dhidi ya Shireen Abu Akleh ripota wa Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kutokuwa ya mwisho. Hapana shaka kuwa, kuna watu wengine ambao watakuwa wahanga wa mauaji ya Israel.