Kuendelea juhudi za Iran za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i88090-kuendelea_juhudi_za_iran_za_kuupatia_ufumbuzi_mgogoro_wa_yemen
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake na mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kwamba, Jamhuri ya Kiislamu daima itaendeleza himaya na uungaji mkono wake kwa irada na matakwa ya wananchi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2022 21:50 UTC
  • Kuendelea juhudi za Iran za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake na mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kwamba, Jamhuri ya Kiislamu daima itaendeleza himaya na uungaji mkono wake kwa irada na matakwa ya wananchi wa Yemen.

Husssein Amir-Abdollahian sambamba na kusisitiza katika mazungumzo yake hayo na Muhammad Abdul-Salaam msemaji wa Harakati ya Ansarullah na mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen kwamba, Tehran inaunga mkono kuongezwa muda wa usitishaji vita ameeleza kuwa, huo ni utangulizi wa kurejeshwa amani ya kudumu na kuonyesha matumaini kwamba, kwa kuondolewa kikamilifu mzingiro wa Yemen faili la masuala ya kibinadamu la nchi hiyo litapata faraja na ahueni.

Kwa upande wake, Muhammad Abdul-Salaam sanjari na kukosoa kutekelezwa nusu nusu usitishaji vita na vilevile ukiukaji ahadi wa upande wa pili amesema kuwa, kuna haja na udharura wa kutekelezwa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la amani.

Kuondolewa mzingiro usio wa kibinadamu dhidi ya wananchi wa Yemen, kutekelezwa usitishaji vita na kusimamishwa vita ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakipigiwa upatu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu Saudi Arabia na washirika wake walipoanzisha hujuma na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen Machi 2015.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Iran ilikuwa nchi ya kwanza kabisa ambayo tangu vita hivyo vilipoanza imekuwa ikitilia mkazo wajibu wa kutatuliwa mgogoro wa Yemen kwa njia ya mazungumzo na daima imekuwa ikisema kuwa, mgogoro huo kamwe hauwezi kutatuliwa kwa mtutu wa bunduki. Kupendekeza mpango wenye vipengee kadhaa unaojumuisha kusitishwa vita haraka iwezekanavyo, kuharakishwa upelekaji misaada ya kibinadamu, kuondolewa mzingiro, mazungumzo baina ya makundi yote ya Yemen na kuundwa serikali jumuishi ya kitaifa ni miongoni mwa hatua za Tehran zinazolenga kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen.

 

Aidha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikifuatilia suala la kufanya mazungumzo na mataifa mengine ya dunia sambamba na kufuatilia kadhia ya Yemen katika asasi na majukwaa ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na imekuwa ikisisitiza kwamba, usitishaji vita tu pekee hautoshi kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen. Hii ni kwa sababu kuna hatua nyingine za ziada hususan kuondolewa mzingiro ambazo zinapaswa kuchukuliwa ili kuweko uwezekano wa kufikishwa misaada ya awali na ya dharura kwa minajili ya kukidhi mahitaji ya kimsingi kwa ajili ya wananchi hao.

Katika hali ambayo, wananchi wa Yemen wanataabika kutokana na kuhitajia pakubwa bidhaa za chakula na nishati ya mafuta, muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala vamizi wa Saudi Arabia umeendelea kuiba mamilioni ya mapipa ya mafuta ya Yemen sambamba na kushikilia na kukwamisha uingiaji wa meli za mafuta katika nchi nchi ya Yemen ambayo kimsingi inahitajia pakubwa bidhaa hiyo.

Isam Mutawakkil, msemaji wa Shirika la Mafuta la Yemen anasema kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukizuia kuingia kwa utaratibu meli za mafuta katika bandari za Yemen na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa hauchukui hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kuhitimisha mzingiro dhidi ya nchi hiyo.

Ukwamishaji mambo huo unaendelea sambamba na ukiukaji wa kila leo wa usitishaji vita unaofanywa na muungano huo vamizi; hatua ambazo zinaonyesha kuwa, Saudia na washirika wake katu si wenye kuheshimu vipengee vya usitishaji vita huku Umoja wa Mataifa nao hauko tayari kuchukua hatua za kuushinikiza muungano huo.

Mauaji msikitini yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia

 

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ambao umeshindwa kufikia malengo yake katika medani ya vita kutokana na kukabiliwa na muqawama na kusimama kidete vikosi vya Yemen na hata kulazimika kukubali mpango wa usishaji vita, umeendelea na vita vya kiuchumi na hivyo kushadidisha mgogoro wa kibinadamu katika nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, hujuma ya kijeshi na kuendelea mzingiro dhidi ya Yemen vimesababisha hasara kubwa ya kimali na kiroho na kupelekea kuharibiwa pakubwa miundomsingi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Filihali wananchi wa Yemen wanakabiliwa na matatizo chungu nzima kama kushindwa kujidhaminia chakula, maji safi na salama ya kunywa na huduma nyingine za afya.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulitangaza hivi karibuni kwamba: Takribani watoto milioni 12 nchini Yemen wanahitajia msaada wa haraka wa chakula na kwamba, hivi sasa nchi hiyo imenasa katika mgogoro mkubwa na wa kutisha wa chakula ambao hivi sasa umeshadidi mno.

Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba, kupatikana usitishaji vita wa kudumu kuna mfungamano na suala la kuondolewa mzingiro kikamilifu. Hii ina maana kwamba, mzingiro wa kibinadamu nchini Yemen unapaswa kuondolewa kikamilifu ili iwezekane kufuatilia kwa njia bora faili la masuala ya kibinadamu katika nchi hiyo.