Bahrain yajiondoa kwenye uchaguzi wa taasisi ya UN kufuatia ukosoaji
Bahrain imelazimika kujiondoa kwenye uchaguzi ujao wa kuwasaka wanachama wapya wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), kufuatia jitihada na lalama za asasi za kutetea haki za binadamu juu ya rekodi nyeusi ya serikali ya Manama.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Bahrain Institute for Rights and Democracy (BIRD) mwezi Agosti mwaka huu lilifanya msururu wa vikao na maafisa wa Umoja wa Mataifa na wanadiplomasia, kushinikiza mataifa yasiunge mkono azma ya Bahrain ya kupewa uanachama katika taasisi hiyo ya haki za binadamu ya UN.
Sayed Ahmed Alwadaei, mkurugenzi wa taasisi ya BIRD amezungumzia hatua hiyo ya Bahrain kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho na kusema: Ni ahueni kubwa kuona Bahrain imejiondoa kufuatiia kampeni zetu athirifu mjini Geneva, za kutaka isipewe uanachama.
Asasi za kutetea haki za binadamu zimetahadharisha mara chungu nzima kuhusiana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa nchini Bahrain na vyombo vya usalama dhidi ya raia na kutaka kukomeshwa vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain (BCHR), nchi hiyo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa miongoni mwa nchi zote za Kiarabu.
Kwa mujibu wa asasi hiyo, vyombo vya usalama vya utawala wa Manama vinawashikilia wafungwa wa kisiasa zaidi ya 4,500 katika jela mbalimbali za nchi hiyo.
Utawala huo wa kiimla umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa utawala wa Saudi Arabia kupambana na maandamano ya umma ya kupigania mageuzi ya kidemokrasia.