Sayyid Hassan Nasrullah: Muqawama ndio njia pekee ya kuikomboa Palestina
Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, umoja wa Kiislamu katika fremu ya muqawama ndio njia pekee ya kukata mikono ya maadui, kuikomboa Palestina na Quds Tukufu na kurejesha adhama na ustahifu wa risala ya Bwana Mtume (saw).
Samahat Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo katika risala yake kwa Mkutano wa 36 wa Kimataifa la Umoja wa Kiislamu unaofanyika hapa mjini Tehran ambayo imesomwa na Sheikh Nabil Qaouk, Mjumbe wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.
Nasrullah amesisitiza katika ujumbe wake huo kwamba, umoja wowote ambao hauko katika mkondo wa kuunga mkono Quds unatia shaka na kwamba, hauna uhusiano na Uislamu.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, hii leo eneo la Asia Magharibi na walimwengu kwa ujumla wanashuhudia kuporomoka haiba na nguvu ya Marekani ambapo kurejea nyuma kwa karibuni kabisa ni kushindwa kwake katika vita huko Iraq, Afghanistan na kunasa katika kinamasi cha vita huko Ukraine.
Aidha katika sehemu nyingine ya risala yake kwa Mkutano wa 36 wa Kimataifa la Umoja wa Kiislamu unaofanyika hapa mjini Tehran Nasrullah amesema: Msimamo wetu wa siku zote ni kuiunga mkono Jamhuri ya kiislamu ya Iran katika kukabiliana na Marekani, utawala haramu wa Israel na vibarakak wao.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amevitaja vikwazo dhidi ya Iran kuwa ni jinai na kupinga hatua zozote za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ambao hufanyika kila mwaka mjini Tehran kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja na kipindi cha kuadhimisha Maulidi na kuzaliwa kwa Mbora wa viumbe, Mtume Muhammad (saw) ulianza rasmi jana kwa hotuba ya Sayyid Ebrahim Raisi.