Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9052-ripoti_ya_umoja_wa_mataifa_kuhusu_jinai_za_utawala_wa_kizayuni
Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu imetoa ripoti inayoeleza kuwa Israel imeua Wapalestina 53 tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2016 09:02 UTC
  • Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni

Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu imetoa ripoti inayoeleza kuwa Israel imeua Wapalestina 53 tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016.

OCHA imebainisha wazi katika ripoti yake hiyo kuhusu jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na kueleza kuwa utawala huo umewauwa shahidi Wapalestina 53 wakiwemo wanawake 5 na watoto 13 tangu kuanza mwaka huu wa 2016, ikiwa ni katika kuendeleza siasa zake za kuwakandamiza na kuwanyanyasa raia wa Palestina wasio na hatia.

OCHA imeashiria katika ripoti yake hiyo kuwa utawala wa Kizayuni unawauwa shahidi raia wa Palestina kwa kuwashuku tu kuwa wanatekeleza oparesheni dhidi ya Wazayuni; na unakataa kuzikabidhi familia mbalimbali miili ya mashahidi tisa wa Intifadha ya Quds waliouliwa na utawala huo.

Ripoti ya Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa wanajeshi wa Kizayuni katika muda wa wiki mbili pekee wamewajeruhi kwa kuwapiga risasi raia 97 wa Kipalestina wakiwemo watoto na wanawake 30 katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na wengine wawili huko Ukanda wa Ghaza.