Ansarullah: Marekani inakwamisha juhudi za kurejesha amani nchini Yemen
Kiongozi wa ngazi ya juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ameishutumu Marekani kuwa inakwamisha juhudi zinazolenga kurejesha amani katika nchi hiyo ya Kiarabu iliyokumbwa na vita.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha habari cha televisheni ya al-Mayadeen cha Lebanon, Abd al-Wahhab al-Mahbashi amesema Marekani inaweka vikwazo katika njia ya kurejesha amani na utulivu nchini Yemen, na kuonya kwamba maslahi ya nchi hiyo katika eneo la Asia Mashariki yatashambuliwa iwapo itaendelea kuunga mkono uvamizi na mzingiro unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen.
Abd al-Wahhab al-Mahbashi amesema: "Wakati uvumilivu wa taifa la Yemen utakapoisha, watatumia chochote walichonacho, ikiwa ni pamoja na silaha na njia nyingine, kutoa pigo kubwa kwa Marekani, ambayo ni adui mkuu na inaunga mkono wavamizi wote nchini Yemen."
Wakati huo huo Yasser al-Houri, Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa, Washington inazishinikiza Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili zizidishe mzingiro wao dhidi ya Yemen.
Saudi Arabia ilianzisha vita vikali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa kushirikiana na washirika wake wa Kiarabu na kwa misaada ya silaha na zana za kivita kutoka Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.
Maelfu ya Wayemeni wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo kutokana na masambulizi hayo.