Iraq yatilia mkazo kuzuia mashambulizi dhidi ya nchi jirani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema kuwa Baghdad ina jukumu la kuzuia mashambulizi ya baadhi ya magenge yenye silaha kutekeleza hujuma dhidi ya nchi jirani kutokea katika ardhi ya nchi hiyo.
Hujuma za karibuni za magaidi wa makundi dhidi ya Mapinduzi katika mipaka ya magharibi mwa Iran zimepelekea ndege zisizo na rubani (droni) na makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kushambulia ngome za magenge hayo ya kigaidi katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan, kaskazini mwa Iraq.
Fuad Hossein Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alisema jana katika mkutano na waandishi wa habari pambizoni mwa Mkutano wa Pili wa Baghdad huko Jordan kwamba: kuna magenge huko Iraq ambayo yanatumia vibaya ardhi ya nchi hiyo kutekeleza mashambulizi dhidi ya nchi jirani na jukumu letu ni kuzuia mashambulizi hayo.
Fuad Hossein aidha amesisitiza kuwa, nchi jirani na Iraq zinapasa kuheshimu mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo na kufungamana na sheria za kimataifa.
Amesema, ili kuzuia hujuma hizo tajwa, nchi yake inawasiliana mara kwa mara na Uturuki na Iran; na kwamba Baghdad imechukua hatua za kuzuia kutumiwa ardhi ya Iraq kuendeshea mashambulizi dhidi ya nchi jirani.