Wananchi wa Bahrain waandamana wakitaka kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i91972-wananchi_wa_bahrain_waandamana_wakitaka_kuachiliwa_huru_wafungwa_wa_kisiasa
Wananchi wa Bahrain wameandamana wakiwaunga mkono wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo na kutoa mwito wa kuachiliwa huru wafungwa hao wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali ya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2022 23:39 UTC
  • Wananchi wa Bahrain waandamana wakitaka kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa

Wananchi wa Bahrain wameandamana wakiwaunga mkono wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo na kutoa mwito wa kuachiliwa huru wafungwa hao wanaoshikiliwa katika magereza mbalimbali ya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara dhidi ya utawala wa kifamilia wa Bahrain na kuutaka uwaachilie huru wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala huo.

Waandamanaji hao wamelaani pia jinai za utawala wa Bahrain na kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na mateso na unyama unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya wananchi wa nchi hiyo wanaopaza sauti zao wakitaka demokrasia ichukue mkondo wake.

Utawala huo wa kiimla umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa utawala wa Saudi Arabia kupambana na maandamano ya umma ya kupigania mageuzi ya kidemokrasia.

 

Tangu wakati huo Bahrain imekumbwa na vuguvugu la harakati za mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka kuwa huru, kutekelezwa uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Wakati huo huo, asasi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimeendelea kutahadharisha kuhusiana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa nchini Bahrain na vyombo vya usalama dhidi ya raia na kutaka kukomesha vitendo hivyo. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hukumu za adhabu ya kifo zimeongezeka mno nchini humo katika muongo mmoja uliopita hasa tangu lilipoanza vuguvugu la Machipuo ya Kiarabu.