Lori la pombe lapinduka Saudia, malalamiko yatanda mtandaoni
Picha za lori lililopinduka likiwa limebeba pombe kwenye barabara moja mjini Riyadh Saudi Arabia zimezua malalamiko mengi kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, kupinduka lori hilo la pombe nchini Saudi Arabia kumezua taharuki kubwa miongoni mwa raia wa nchi hiyo huku watu mbalimbali wakisambaza picha na video zinazoonesha lori lililobeba pombe likiwa limepinduka katika wilaya ya Qairawan mjini Riyadh.
Video iliyoenea sana kwenye mitandao ya kijamii inaonesha idadi kubwa ya chupa za pombe kali zilizomwagika chini baada ya lori hilo kupinduka. Lori hilo lilikuwa likisafiri kwenye barabara ya pembeni na si kwenye barabara kuu kabla ya kupinduka.
Watu wengi wameonekana karibu na eneo la tukio lakini vyombo vya usalama havikuonekana kabisa kwenye video hiyo.
Mwanaharakati maarufu wa Saudia, Turki Al-Shalhoub naye ameweka picha kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema, gari lililokuwa limebeba pombe limepinduka katika moja ya mikoa ya nchi yetu.
Hivi majuzi, jarida la Biashara la Arabia lilitangaza kuwa serikali ya Saudi Arabia inapanga kuruhusu uuzaji wa vileo na pombe katika maeneo yasiyolipiwa ushuru kwenye viwanja vya ndege.
Hapo awali, gazeti la "Wall Street Journal" lilifichua kuwa Saudi Arabia inapanga kuruhusu uuzaji wa aina mbalimbali za pombe katika kisiwa cha "Sindalah" kilichoko Neom.
Mwanzoni mwa 2020, Mohamad Bin Salman mrithi wa ufalme wa Saudia ambaye ndiye hasa anayeongoza nchi hiyo hivi sasa aliamua kuingiza pombe katika hoteli za Saudia kwa kisingizio cha mkutano wa G20. Duru za kifalme zilisema, kazi ya kuingiza pombe nchini Saudia imepewa kampuni ya "Al-Hakir."