Dec 28, 2022 08:03 UTC
  • Mohammad Shtayyeh
    Mohammad Shtayyeh

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema: Tangu mwanzoni mwa mwaka huu utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 220 katika maeneo tofauti ya Palestina.

Akizungumza katika kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mohammad Shtayyeh, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema, tangu mwanzoni mwa mwaka huu utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 220, kujeruhi watu 9,000 na wengine 6,500 wametiwa nguvuni katika maeneo mbalimbali ya Paslestina.

Shtayyeh ameongeza kuwa, mwaka huu (2022) utawala wa Kizayuni umeharibu majengo 832 na kung'oa mizeituni 13,000 ya Wapalestina.

Mamia ya Wapalestina wameuawa mwaka huu wa 2022

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kuwa, wananchi wa ardhi hiyo walikabiliana kwa ushujaa na hujuma za kikatili za utawala wa Kizayuni na wanaendelea kusimama kidete kukabiliana na uvamizi wowote dhidi ya ardhi na nchi yao na kulinda harakati za ukombozi wa taifa kwa kujitolea muhanga.

Shtayyeh amesema kuwa watu wa Palestina mwaka huu pia walikabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi kutokana na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa misaada ya kimataifa, kuendelea kwa makato ya kodi kunakofanywa na Israel kutoka kwa Wapalestina, matokeo ya janga la Corona na vita vya Ukraine. Amesisitiza kuwa hata hivyo, Palestina ikilinganisha kwa nchi nyingi, imekuwa na ustawi wa juu wa uchumi.

Tags