Saudia yaialika timu ya UN ili kujaribu kupotosha fikra za waliowengi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9274-saudia_yaialika_timu_ya_un_ili_kujaribu_kupotosha_fikra_za_waliowengi
Saudi Arabia imeialika timu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mazungumzo baada ya kuushinikiza umoja huo uondoe jina lake katika orodha nyeusi ya wakiukaji wa haki za watoto.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2016 23:21 UTC
  • Saudia yaialika timu ya UN ili kujaribu kupotosha fikra za waliowengi

Saudi Arabia imeialika timu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mazungumzo baada ya kuushinikiza umoja huo uondoe jina lake katika orodha nyeusi ya wakiukaji wa haki za watoto.

Abdullah al Mouallimi, Balozi wa Saudia katika Umoja wa Mataifa amewasilisha mwaliko huo rasmi kupitia barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wiki iliyopita. Stephene Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa wanasubiri kuona ni taarifa ipi watapokea kutoka kwa muungano vamizi nchini Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia.

Saudi Arabia na Umoja wa Mataifa kwa pamoja zilikabiliwa na ukosoaji kutoka pembe mbalimbali za dunia baada ya Katibu Mkuu wa umoja huo kukiri kuwa ameliondoa jina la Riyadh kwenye orodha nyeusi ya umoja huo kutokana na mashinikizo. Umoja wa Mataifa ulisema kuwa kuondolewa jina la Saudia ilikuwa ni kwa muda mfupi tu kwa kuwa wanasubiri kufanyika mazungumzo ya pande mbili ili kupitia upya ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuuliwa watoto wa Yemen katika mashambulizi ya anga ya ndege za kivita za Saudia. Itakumbukwa kuwa, Umoja wa Mataifa ulichapisha ripoti yake tarehe 3 mwezi huu iliyoeleza kuwa, Saudi Arabia imehusika na asilimia 60 ya vifo vya watoto wa Yemen mwaka uliopita, ambapo watoto 510 waliuliwa na wengine 667 walijeruhiwa.