Sana'a: Uingereza sababu kuu ya uvamizi Yemen
Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameeleza kuwa, Uingereza si tu haiwezi kusaidia kupunguza mateso na masaibu ya kiuchumi ya wananchi wa Yemen bali nchi hiyo ni sehemu kuu ya njama ya kuvamiwa nchi hiyo.
James Kariuki mwanadiplomasia wa serikali ya Uingereza ambaye ni Naibu Balozi wa Kudumu wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ameitolea wito jamii ya kimataifa eti kutekeleza hatua zote ili kupunguza athari za kiuchumi na kuisadia serikali ya Yemen katika kipindi hiki nyeti kufuatia madai kwamba zuio la kuuza mafuta ililowekewa harakati ya Ansarullah limeisababishia serikali ya Yemen mbinyo wa kiuchumi.
Abdulaziz bin Habtoor Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameeleza kuwa, matamshi ya karibuni ya Balozi huyo wa Uingereza si ya kuwajibika na kwamba uamuzi wa serikali kibaraka ya Yemen ya kuongezeka tozo la ushuru wa forodha kwa sarafu ya dola katika kipindi hiki ni dhidi ya wananchi wote wa Yemen.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameongeza kuwa, hadi kufikia leo Uingereza imehusika pakubwa katika kuvamiwa Yemen kwa upande wa kuratibu mipango na vitendo na kusisitiza kuwa London ndiyo inayoilinda serikali mamluki.
Sana'a aidha imeutolea wito Umoja wa Mataifa na wapigania amani na ukombozi duniani kulaani uingiliaji wa wazi wa Uingereza katika masuala ya ndani ya Yemen; wenye lengo la kutoa pigo kwa amani ya Yemen. Serikali ya Yemen imetaka kuwepo tathmini ya kiadilifu kuhusu hali ya kiuchumi ya Yemen ili kuhitimisha matatizo ya kibinadamu kwa watu wa nchi hiyo.