Uhispania yamuita nyumbani balozi wake wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130626-uhispania_yamuita_nyumbani_balozi_wake_wa_israel
Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa Uhispania imemuita tena balozi wake katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ikilalamikia sera za mauaji za Israel katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-09-10T06:40:01+00:00 )
Sep 10, 2025 06:40 UTC
  • Uhispania yamuita nyumbani balozi wake wa Israel

Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa Uhispania imemuita tena balozi wake katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ikilalamikia sera za mauaji za Israel katika Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la Reuters liliandika siku ya Jumatatu kwamba Uhispania ilimwita balozi wake wa Israel. Madhumuni ya hatua hii ya Uhispania imetangazwa kama ni mashauriano na balozi. Serikali ya Uhispania pia ilikanusha tuhuma za utawala wa Kizayuni wa chuki dhidi ya Wayahudi.

Serikali ya Madrid imebainisha kuwa maamuzi ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu Pedro Sanchez kuhusu hali ya kinyama huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yako ndani ya mfumo wa kutetea amani na haki za binadamu. Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, ametangaza hatua mpya kali za kidiplomasia na kiusalama zenye lengo la kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili usitishe mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

 Sanchez amesema kuwa serikali ya Madrid itapiga marufuku meli na ndege zinazobeba silaha au mafuta kwa ajili ya Israel kuingia katika anga ya Hispania au kutia nanga katika bandari zake.

Madrid pia imeahidi kuongeza msaada kwa Mamlaka ya Palestina na Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kwa kiasi cha euro milioni 10, pamoja na euro milioni 150 za ziada kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa Gaza ifikapo mwaka 2026.

Kabla ya hapo, Yolanda Diaz, Naibu Waziri Mkuu wa Pili wa Uhispania na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Kijamii, alikuwa amesisitiza ulazima wa kusitishwa mikataba yote na kusimamisha biashara na utawala wa Kizayuni ili kukabiliana na "uchumi wa mauaji ya kimbari."