Iran yataka hatua zichukuliwe kukomesha jinai ya Israel dhidi ya Wapalestina
Iran imeitaja kambi ya wakimbizi ya Jenin kama ngome ya muqawama au mapambano na imeitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka kukomesha jinai za utawala haramu wa Israel baada ya utawala huo kuua Wapalestina 10 siku ya Alhamisi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Hossein Amir-Abdollahian aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter siku ya Ijumaa kwamba, "Shambulio la kikatili la utawala wa Kizayuni na mauaji ya Wapalestina katika kambi ya Jenin linahitaji hatua za haraka za jumuiya ya kimataifa na nchi za Kiislamu dhidi ya wahalifu."
"Jenin imegeuka kuwa ngome ya muqawama (mapambano), na hakuna shaka katika suala hili."
Hapo awali Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani vikali shambulio la kikatili la wanajeshi wa Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jenin na kusababisha vifo vya Wapalestina kadhaa.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Nasser Kan’ani alisema kutochukua hatua na kunyamaza kwa mashirika husika ya kimataifa na wale wanaojiita watetezi wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi kuhusu jinai za kila siku zinazofanywa na utawala wa Tel Aviv ni jambo chungu na la aibu.
Kan’ani pia amezitaka nchi za Kiislamu kuchukua msimamo mmoja na kuchukua hatua katika kuwalinda wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na mapambano ya halali dhidi ya wavamizi Wazayuni
Siku ya Alhamisi, wanajeshi wa Israel waliwaua Wapalestina 10 katika moja ya siku mbaya zaidi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu tangu mashambulizi ya Israel yalipoanza mwanzoni mwa mwaka jana.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, Wapalestina tisa waliouawa walikuwa katika kambi ya wakimbizi ya Jenin, baada ya majeshi ya Israel kuvamia eneo hilo.
Mpalestina mwingine mwenye umri wa miaka 22 alipigwa risasi na wanajeshi wa Israel katika mji wa al-Ram, kaskazini mwa Al Quds (Jerusalem).
Katika uvamizi wa Jenin, ambao Wapalestina wameutaja kama "mauaji ya umati", takriban Wapalestina wengine 20 walijeruhiwa kwa risasi za moto.