Wazayuni saba waangamizwa Palestina kaskazini ya Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu
Jan 28, 2023 04:33 UTC
Duru za habari zimeripoti usiku wa kuamkia leo kuwa, Wazayuni saba wameangamizwa kwa kupigwa risasi kaskazini mwa mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, chaneli ya 13 ya televisheni ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel imeripoti kuwa, walowezi saba wameangamizwa kufuatia ufyatuaji risasi uliotokea katika eneo la An-Nabiyyu-Yaaqub, lililoko kaskazini mwa Quds.
Vyanzo vya Kizayuni vimetangaza kuwa watu 12 walijeruhiwa pia katika shambulio hilo la ufyatuaji risasi.
Polisi wa Kizayuni wamemuua shahidi mmoja wa wahusika wa shambulio hilo huku wakiendelea kuwatafuta wahusika wengine.
Wazayuni hao saba wameangamizwa wakati siku ya Alkhamisi wanajeshi wa Kizayuni walishambulia kambi ya wakimbizi Wapalestina katika mji wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambako waliwaua shahidi Wapalestina kumi na kuwajeruhi wengine 20.
Katika kujibu jinai hiyo, vikosi vya muqawama wa Palestina vilifyatua makombora kadhaa kuelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Wakati huo huo, mamia ya Wapalestina wakiongozwa na viongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana Ijumaa walifanya maandamano na mkusanyiko mkubwa kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa mji wa Jenin na kulaani hujuma na uvamizi wa adui Mzayuni katika mji huo.../