Iran, Uturuki, Russia zasisitiza kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala Syria
Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Uturuki, Russia na Syria wamesisitiza kulindwa mipaka na mamlaka ya kitaifa ya kujitawala Syria na kutoingiliwa masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Mawaziri hao pia wamezindua ramani ya njia ya kuboresha uhusiano uliodorora kati ya Syria na Uturuki katika mkutano katika mji mkuu wa Russia, Moscow.
Wanadiplomasia hao wakuu waliyasema hayo Jumatano katika taarifa ya mwisho mwishoni mwa mkutano wa pande nne uliolenga kufikiwa maridhiano na kurejesha uhusiano kati ya Syria na Uturuki katika nyanja mbalimbali.
Aidha wameeleza dhamira yao ya kupambana na aina zote za ugaidi, harakati za kutaka kujitenga na misimamo mikali nchini humo.
Mawaziri hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuongeza misaada ya kibinadamu ya kimataifa kwa Syria kwa lengo la kuwezesha kurejea kwa hiari, salama na kwa heshima kwa Wasyria katika nchi yao na ujenzi mpya wa baada ya vita.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwisho, washiriki walikubaliana kwamba manaibu mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo nne wanapaswa kutekeleza jukumu la kuandaa ramani ya kuendeleza uhusiano kati ya Uturuki na Syria kwa uratibu wa wizara za ulinzi za nchi hizo nne na wakuu wa idara za usalama.
Uturuki ilikata uhusiano wake na Syria mnamo Machi 2012, mwaka mmoja baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kujabiliwa na ghasia zilizoendeshwa na wanamgambo na magaidi waliokuwa wakipata uungaji mkono wa madola ya kigeni, wakiwemo wale wanaoungwa mkono na Ankara.
Nchi hizo mbili jirani kwa sasa zinachukua hatua kuelekea maridhiano baada ya miaka 11 ya kuharibika uhusiano.
Katika jitihada za mwisho za kurekebisha uhusiano kati ya Ankara na Damascus, mawaziri wa ulinzi na wakuu wa upelelezi wa Russia, Syria, Uturuki na Iran walikutana mjini Moscow mwishoni mwa mwezi uliopita na kujadili kuhusu kuondolewa wanajeshi wa Uturuki nchini Syria.
Mchakato wa kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Ankara na Damascus ulianza Desemba 28, 2022, wakati mawaziri wa ulinzi wa Russia, Syria na Uturuki walipokutana mjini Moscow.
Rais wa Syria Bashar al-Assad alisema mwezi Januari kwamba maelewano na Uturuki yatategemea Uturuki kuacha kukalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Syria na uungaji mkono wake kwa makundi ya wapiganaji wanaopigana dhidi ya serikali ya Damascus.