Jihadul- Islami:Hujuma yoyote dhidi ya Quds; itavuruga milingano yote
Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina imesisitiza kuwa sera za jinai za adui Mzayuni dhidi ya Quds na Msikiti wa Al-Aqsa zinafanyika katika fremu ya vita vya kidini vya utawala huo dhidi ya taifa la Palestina.
Itamar Ben-Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni, leo asubuhi alivamia katika Msikiti wa Al-Aqsa na kisha kuingia katika eneo la Bab al-Maghreb. Hujuma hiyo ya uvamizi imetekelezwa kwa kuungwa mkono pakubwa na wanajeshi wa Kizayuni; ambapo Be-Gvir baada ya kupita katika maeneo tofauti ya Msikiti wa Al-Aqsa, aliekekea katika eneo la ukuta wa Buraq (mahali ambapo sherehe za kidini za Wazayuni hufanyika).
Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala ghasibu wa Israel amedai katika hotuba yake baabda ya kuuvamia msikiti wa al Aqsa kwamba, na hapa ninamnukuu:" Sisi ni wamiliki wa Quds." Shirika la habari la Shihab imeripoti kuwa, Harakati ya Jihadul-islami ya Palestina leo imetangaza kuwa uvamizi wowote dhidi ya Quds utabadili milingano yote na kwamba njia pekee ya kukabiliana na uchokozi wa iana hiyo itakuwa ni muqawama.
Mushir al Masri mwakilishi wa Bunge la Palestina na mmoja wa viongozi wa Harakati ya Hamas pia amesema kuwa kufanyika kikao kila wiki cha baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni katika njia za chini kwa chini zilizoko chini ya eneo la ukuta wa Buraq ni sawa na kutangaza kivita, na ni hatua inayodhihirisha fikra za uchupaji mipaka na kupenda chokochoko Wazayuni maghasibu.
Leo pia baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni katika hatua yake ya uchokozi limefanya kikao chake kwa mara ya pili tangu mwaka 2017 katika eneo la chini la Msikiti wa Al-Aqsa. Hujuma na hatua za kichokozi za Wazayuni za kuuvamia pakubwa msikiti wa al Aqsa ambazo zilishadidi sambamba na kuanza mwezi Mtukufu wa Ramadhan zingali zinaendelea.