Timu ya vitara (fencing) ya Iraq yakataa kushindana na Israel
Timu ya taifa ya vitara (fencing) ya Iraq imejiondoa katika michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2023 ya Shirikisho la Kimataifa la Vitara (FIE) katika mji wa Istanbul nchini Uturuki baada ya kubaini kwamba italazimika watalazimika kukabiliana na timu ya utawala haramu wa Israel.
"Timu ya taifa ya Iraq ilijiondoa katika shindano la binafsi katika Mashindano ya Dunia ya Vitara, yanayoendelea Istanbul na ni ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris, baada ya bahati nasibu kuipanga kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel," Shirikisho la Mchezo wa Vitara la Iraq limesema katika ukurasa wa Facebook.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Uamuzi wa kujiondoa ulikuja kwa kufuata sheria inayoharamisha uhalalishaji wa mahusiano na Israel kama ilivyoidhinishwa na bunge la Iraq, kwa kukataa chombo kinachokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuonyesha mshikamano na taifa la Palestina."
Bunge la Iraq lilipitisha sheria mnamo Mei 2022, kupiga marufuku aina yoyote ya hatua za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheria hiyo inatumika kwa raia na maafisa wote wa Iraq pamoja na taasisi zinazosimamiwa na serikali na pia katika vyombo vya habari.
Haya yanajiri siku chache baada ya mchezaji vitara wa Kuwait, Abdulaziz Alshatti, pia kutangaza uamuzi wake wa kujiondoa katika mashindano hayo ili kuepusha kukabiliana na mshiriki wa utawala haramu wa Israel.
Sawa na Iraq, Bunge la Kuwait liliidhinisha kwa kauli moja miswada ya sheria mnamo Mei 2021, ikiharamisha mikataba au hatua yoyote inayoashiria kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Hii si mara ya kwanza kwa wanamichezo wa Kiislamu kutoka katika ulimwengu wa Kiislamu kukataa kukabiliana na washindani wa Israel katika matukio mbalimbali ya michezo wakipinga jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina katika ardhi za Palestina ambazo unazikalia kwa mabavu.
Nchi za Kiislamu zinautazama ushiriki wa wanamichezo wa Israel katika matukio ya michezo kuwa ni mpango wa kuusaidia utawala wa Tel Aviv hatua kwa hatua kurejesha uhusiano wake na mataifa ya Kiislamu na Kiarabu licha ya kuikalia kwa mabavu Palestina na jinai zake zisizo na kikomo dhidi ya Wapalestina.
Aprili mwaka jana, Eyas al-Zamer, kijana mcheza vitara wa Jordan alijiondoa katika Mashindano ya Dunia ya Uzio wa Vijana katika Umoja wa Falme za Kiarabu ili kuepuka kushindana dhidi ya mwanariadha wa Israel.