HAMAS: Israel inataka kuwafunga jela watoto zaidi wa Palestina
(last modified Sun, 18 Jun 2023 07:39:56 GMT )
Jun 18, 2023 07:39 UTC
  • HAMAS: Israel inataka kuwafunga jela watoto zaidi wa Palestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani njama zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kupasisha sheria inayoruhusu kufungwa jela watoto wadogo wa Kipalestina wa kuanzia miaka 12.

Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na HAMAS imeeleza kuwa, muswada wa sheria hiyo unaojadiliwa hivi sasa katika Bunge la Kizayuni (Knesset) unaonyesha wazi sura halisi na dhati ya ukatili na ubaguzi wa Wazayuni.

Imesema: Watoto wa Kipalestina daima wamekuwa wahanga wa jinai za kihaini za Wazayuni kupitia uvamizi na ugaidi, sanjari na kuwatesa, kuwakamata na hata kuwaua watoto hao.

HAMAS imesema vita vya utawala huo haramu dhidi ya watoto wa Kipalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu vinafanyika kupitia jinai za utekaji nyara, kukamatwa, kuuawa kwa kufyatuliwa risasi, kufungiwa majumbani na kuwatumia watoto wa Palestina kama ngao za binadamu.

Hivi karibuni, HAMAS ilitoa wito wa kutambuliwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watoto wa Kipalestina kuwa ni uhalifui na jinai, na kutaka kufunguliwa mashitaka wanaofanya jinai hizo.

Askari wa Kizayuni wanavyoamiliana na watoto wa Palestina

Kwa mujibu wa harakati hiyo ya muqawama, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watoto na barobaro 28 wasio na hatia wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala huo.

HAMAS imesema kimya cha jamii ya kimataifa na kutotambua uhalifu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina kuwa ni jinai, na vilevile mienendo ya kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na kadhia hiyo ni sawa na kuwaruhusu maafisa wa utawala huo na serikali yake ya kifashisti kufanya vitendo zaidi vya kigaidi dhidi ya watoto wasio na hatia.

Tags