Hamas: Mustakabali wa giza unaungojea utawala wa Kizayuni wa Israel
Mwanachama wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas amesema: Mustakhbali mbaya na wa giza unaungojea utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba kupanuka kwa muqawama na mapambano ni ishara ya mustakbali mbaya wa Israel.
Salah Al-Bardawil, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema: "Muqawama na mapambano ya Jenin, safu ya mashambulizi ya wanamapambano na matukio ya sasa, ni utangulizi wa mlipuko wa pande zote."
Akiashiria kwamba mapambano ya Wapalestina wa Jenin yataongezeka kutokana na irada ya wanamuqawama, Al Bardawil amesema, Hamas inaona fahari kuhusishwa na medani za vita na kwamba Gaza haitaacha kushiriki katika medani zote za vita vya ukombozi wa Palestina.
Afisa huyo wa Hamas amesema kuwa, Gaza inaunga mkono mapambano ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuongeza kuwa, tangu mwaka 2007 Ukingo wa Magharibi umekuwa chini ya mashinikizo ya Israel na walowezi wa Kizayuni.
Huku akisema jinai za Wazayuni zinaakisi hofu yao kubwa mbele ya watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Salah Al-Bardawil ametangaza kuwa: Muqawama wa Ukingo wa Magharibi unapaswa kuchukua stratijia itakayoutia kiwewe utawala haramu wa Israel.
Katika mashambulizii yake ya karibuni dhidi ya raia wa Palestina kwenye mji wa Jenin, utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua shahidi Wapalestina 12 na kujeruhi wengine 140. Jeshi la Israel lililazimika kuondoka katika eneo hilo masaa 48 baadaye kutokana na muqawama na mapambano ya kishujaa ya vijana wa Kipalestina.