Jul 25, 2023 07:08 UTC
  • Russia: Dunia haiwezi tena kuvumilia sera za kutii amri za Marekani

Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema dunia ya sasa haivumilii tena sera za kufuata amri za Marekani na inaelekea kwenye mfumo wa kambi kadhaa, mchakato ambao haukubaliwi na nchi za Magharibi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tass, Nikolay Patrushev, ameyasema hayo katika mkutano wa maafisa wakuu wa usalama wa nchi wanachama wa BRICS uliofanyika nchini Afrika Kusini na kubainisha kwamba nchi za Magharibi zinajaribu kuzitumia kwa manufaa yao sheria za Umoja wa Mataifa na kuyabebesha sheria hizo akthari ya mataifa ya ulimwengu. Patrushev ameongeza kuwa, katika usanifu wa kisiasa na kiuchumi wa dunia ya zama hizi, kuna maombi yanayoongezeka ya kuongezwa uwakilishi wa nchi za Asia, Afrika, Amerika ya Latini na Magharibi ya Asia zinazofuata siasa na sera huru katika mambo yao ya nje na ambazo ziko tayari kutetea maslahi yao ya kitaifa na mamlaka yao ya utawala katika taasisi za utawala za kimataifa.

Mwaka huu wa 2023, Afrika Kusini ndiyo inayoongoza kundi la nchi wanachama wa BRICS, ambapo mkutano wa 13 wa maafisa wakuu wa usalama wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo unafanyika nchini humo.

 
Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini ndizo wanachama wakuu wa kundi la BRICS.../

 

Tags