Sisitizo la kufanyiwa mabadiliko muundo wa Umoja wa Mataifa
-
Antonio Guterres
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesisitiza haja ya kufanyiwa mabadiliko muundo wa umoja huo na kuonya kuwa, huenda kukajitokeza mgawanyiko iwapo jambo hilo halitazingatiwa.
Huku akiashiria kuanza mfumo wa kambi kadhaa katika kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Guterres amesisitiza ulazima wa kuwepo mabadiliko katika Umoja huo kutokana na kukosekana uwiano wa kisiasa duniani.
Onyo hilo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa linatolewa wakati ambapo umoja huo, hasa katika kipindi cha hivi karibuni, umekuwa ukikabiliwa na shutuma nyingi kutokana na udhaifu wa mfumo na sera zake katika kukabiliana na matukio umuhimu ya kimataifa.
Kuibuka nguvu mpya za kisiasa na kiuchumi, mabadiliko katika mfumo wa kimataifa, migogoro ya kikanda na vita, janga la Covid-19 na athari zake katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi ulimwenguni vimezidisha haja ya kuwepo mabadilisha katika muundo wa Umoja wa Mataifa.
Katika miongo ya hivi karibuni, madola makubwa na yenye ushawishi, ambayo ni mihimili mikuu ya Baraza la Usalama, yamedhoofisha nguvu na uwezo wake kwa kupitisha sera zinazokwenda kinyume na maazimio na mapendekezo ya jumuia hiyo ya kimataifa. Hatua hiyo imepelekea wanachama wengi kutozingatia wala kuyapa umuhimu mapendekezo hayo. Baadhi ya wanachama muhimu wa Baraza la Usalama la UN, kama Marekani, hawalipi ada zao za uanachama kwa ukamilifu na kwa wakati, na hutoa mashinikizo dhidi ya baraza hilo kwa maslahi yao binafsi. Donald Trump, rais wa zamani Marekani, aliiondoa nchi hiyo katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na kukataa kulipa ada ya uwanachama kwa madai kwamba, shirika hilo lilichukua misimamo ya chuki dhidi ya utawala haramu wa Israeal.
Kwa upande mwingine, muundo wa Umoja wa Mataifa haujasasishwa kwa miaka mingi licha ya kuwa mfumo wa kimataifa umepitia mabadiliko muhimu na makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na hayo baadhi ya wanachama wanazuia kufanyika mabadiliko ya kisera na kimuundo ambayo yataenda sambamba na hali mapya ya kimataifa.
Kuongezeka mivutano na tofauti kati ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusiana na vita vya Ukraine pamoja na ushindani wa kisiasa na kibiashara wa Magharibi, Russia na China unaoongezeka kila siku, hakujatoa matumaini ya kufanikishwa malengo ya Umoja wa Mataifa, kwa kadiri kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekiri waziwazi kuwa umoja huo hauna tena uwezo wala pesa za kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Richard Govan, Mkurugenzi wa Kundi la Migogoro ya Kimataifa la Umoja wa Mataifa, pia anasema, hali ya Umoja wa Mataifa ni mbaya sana kadiri kwamba umoja huo umefika kwenye ukingo kutokana na kuatharika na mivutano na tofauti kubwa za kidiplomasia zinazozidi kushuhudiwa ndani ya taasisi hiyo ya kimataifa.
Kuendelea kudhoofika Umoja wa Mataifa, kunayaathiri zaidi mataifa madogo na dhaifu kuliko yale yenye nguvu, kutokana na vita, uingiliaji wa kigeni au hata mabadiliko ya hali ya hewa na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza yaliyoratibiwa na kuenezwa na mashirika ya kijinai ya kimataifa.