Polisi ya Ujerumani yavamia vituo 54 vya Kiislamu
(last modified Sat, 18 Nov 2023 03:49:03 GMT )
Nov 18, 2023 03:49 UTC
  • Polisi ya Ujerumani yavamia vituo 54 vya Kiislamu

Jeshi la polisi la Ujerumani juzi Alkhamisi lilishambulia vituo zaidi ya 50 vya Waislamu kikiwemo Kituo cha Kiislamu cha Hamburg (IZH); huku mashambulio ya kibaguzi dhidi ya Waislamu yakiripotiwa kukithiri katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Shirika la habari la Mehr liliripoti habari hiyo jana Ijumaa na kueleza kuwa, askari polisi wa Ujerumani siku ya Alkhamisi walivamia vituo 54 vya Waislamu, kwa kisingizio cha kufanya uchunguzi.

Polisi ya Ujerumani inadai kuwa iliendesha operesheni hiyo dhidi ya vituo vya Kiislamu kote nchini, kwa madai kuwa Kituo cha Kiislamu cha Hamburg eti kinaunga mkono shughuli za Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser amedai kuwa, serikali ya Berlin kamwe haitaruhusu kile alichokitaja kuwa 'propaganda za Kiislamu', chuki dhidi ya Uyahudi na chuki dhidi ya Israel.

Hii ni katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni, nchi nyingi za Magharibi ikiwemo Marekani, Uingereza na hata huko Ujerumani kwenyewe, kumeshuhudia maandamano ya kulaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Ujerumani

Waislamu nchini Ujerumani wanaendelea kuandamwa na mashambulizi ya kibaguzi. Jumla ya matukio 898 ya chuki dhidi ya Uislamu yalirekodiwa nchini humo mwaka jana 2022, huku idadi ya kesi ambazo hazikuripotiwa ikiwa kubwa. 

Aidha takwimu za hivi karibuni za Kituo cha Utafiti wa Utangamano na Uhamiaji cha Ujerumani (Dezim) zinaonesha kuwa, asilimia 41.2 ya wanaume wafuasi wa dini ya Kiislamu nchini humo wanaandamwa na ubaguzi kila siku kwa misingi ya imani yao.

Aidha utafiti huo wa Dezim umefichua kuwa, asilimia 46 ya wanawake Waislamu nchini humo wanakabiliwa na aina moja au nyingine ya ubaguzi kila siku katika ofisi za umma na taasisi za serikali.