Dec 03, 2023 06:41 UTC
  • EU yazidisha tena kiwango cha kununua fueli nyuklia kutoka Russia licha ya kudai kuiwekea vikwazo vikali Moscow

Shirika la Nishati ya Atomiki la Barani Ulaya limetangaza kuwa, nchi za bara hilo zimeongeza kiwango cha kununua fueli nyuklia kutoka kwa Russia licha ya kuiwekea vikwazo nchi hiyo kwa madai ya vita vya Ukraine.

Kwa mujibu wa Reuters, shirika hilo la nishati ya atomiki la Ulaya limedai kuwa fueli nyuklia haimo kwenye orodha ya vikwazo vya nchi za Magharibi kwa Russia.

Kaimu wa shirika hilo la ESA amenukuliwa na shirika hilo la habari la Uingereza akisema kuwa, mwaka huu wa 2023, nchi za Ulaya zimeongeza kiwango cha manunuzi ya fueli nyuklia ya Russia inayozalishwa na kinu cha WER ikilinganishwa na mwaka 2021.

Amesema, mwaka jana 2022, Bulgaria Jamhuri ya Czech, Finland, Hungary na Slovakia ziliongeza kiwango cha manunuzi yao ya fueli nyuklia kutoka Russia. 

Licha ya nchi za Magharibi kuiwekea vikwazo vikali Moscow, lakini bado ni tegemezi sana kwa nishati ya Russia

 

Kabla ya hapo, yaani mwezi ulioisha wa Novemba, Kathryn Huff, Mkuu wa Ofisi ya Nishati ya Atomiki ya Wizara ya Nishati ya Marekani alisema kuwa, utegemezi wa Washington kwa fueli nyuklia ya Russia ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa wa nchi hiyo.

Alisema, kitu kinachotia wasiwasi zaidi kuliko jambo jingine lolote ni kwamba, karibu asilimia 20 ya fueli inayotumiwa na vinu vya nyuklia vya Marekani inanunuliwa kutoka Russia.

Mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, televisheni ya Bloomberg iliripoti kuwa, nchi za Ulaya na Marekani zimefanya juhudi kubwa za kutafuta mbadala wa urani na nishati ya Russia lakini zimeshindwa na inavyoonekana zitaendelea kwa miaka mingi kuwa tegemezi kwa nishati ya Russia.

Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, karibu nusu ya nishati ya urani duniani inadhaminiwa na Russia.