Dec 20, 2023 02:37 UTC
  • Kujiandikisha Putin kwa ajili ya uchaguzi wa Russia 2024

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amethibitisha hhatua ya kwenda Rais Vladimir Putin wa Russia katika Kamati Kuu ya Uchaguzi ya nchi hiyo na kujiandikisha kama mgombea kwa muhula ujao wa urais, ambao utafanyika katikati ya Machi 2024. Putin amewasilisha stakabadhi zinazohitajika ili kujiandikisha kuwa mgombea urais.

Hapo awali, Putin alitangaza utayari wake wa kugombea katika uchaguzi ujao wa rais katika hafla iliyohudhuriwa na zaidi ya shakhsia wa kijeshi na mashujaa 200 wa nchi hiyo.  Muhula wa sasa wa urais wa Putin unatarajiwa kumalizika Mei 7, 2024. Hii itakuwa mara ya tano kwa Putin kushiriki katika uchaguzi kama mgombea wa kiti cha urais. Ikiwa atashinda duru hii ya uchaguzi, basi muhula wake wa urais utadumu kwa miaka mingine 6 yaani ataendelea kuiongoza nchi hiyo hadi 2030. Vladimir Putin alizaliwa Oktoba 7, 1952 na ndiye rais wa sasa wa Russia. Aidha Putin ndiye mkuu wa Chama cha United Russia tangu Aprili 15, 2008.

Vladimir Putin amekuwa akishikilia wadhifa wa rais au Waziri Mkuu wa Russia tangu mwaka 1999. Mnamo 2000, Putin kwa mara ya kwanza alikuwa rais wa Shirikisho la Urusi na kwa miaka minne. Kisha alichaguliwa tena mnamo 2004 na akashikilia wadhifa huo hadi 2008. Baada ya hapo, amekuwa rais wa Russia tangu 2012 na atashikilia wadhifa huu hadi 2024.

Kulingana na moja ya vifungu vya katiba vilivyofanyiwa marekebisho mnamo 2020, kikomo cha muhula wa urais kinatumika bila kujali duru alizoongoza Putin huko nyuma. Hii ina maana kwamba anaweza kushiriki katika uchaguzi wa urais kwa mihula mingine miwili. Katiba ya awali haikuwa ikimruhusu rais wa Russia kuongoza kwa zaidi ya mihula miwili mtawalia. Lakini sheria mpya ya sasa uchaguzi wa rais nchini Russia, ambayo ilipasishwa na bunge baada ya kura ya maoni ya marekebisho ya katiba na kutiwa saini na Putin mwenye akiwa Rais, inamruhusu kushikilia wadhifa wa rais bila kizuizini hadi 2036. Mnamo Julai 2020, wananchi wa Russia walipiga kura kuunga mkono marekebisho ya Katiba ya nchi hiyo.

Rais Putin akijaza fomu za kugombea kiti cha urais katika uchaguzi ujao 2024

 

Shuaib Bahman, mtaalamu wa masuala ya Russia, anasema: Mchakato wa mabadiliko na marekebisho katika katiba ya Russia utaunda na kuleta hali ambayo kupitia kwayo, machaguo mengine yaani chaguo la mrithi wa Putin, litapungua sana, na bado anaweza kuwa mtu nambari moja na mchukuaji maamuzi mkuu katika nchi hiyo ambaye ataendelea kubakia madarakani.

Kwa kufanyika marekebisho ya katiba ya Russia, Putini amesafishiwa njia ya kuendelea kutawala nchini humo hadi mwaka 2036.

Suala hili hakika ni habari mbaya kwa wapinzani wa ndani wa Putin na wafuasi wao wa Magharibi. Akiwa rais mwenye nguvu, ushawishi na ufanisi, kinyume na mtazamo wake wa awali, Putin amefikia hitimisho kwamba iwapo mamlaka nchini Russia yatamfikia mwanasiasa mwingine katika uchaguzi wa urais wa 2024, licha ya hatua zote alizochukua katika fremu ya mageuzi ya katiba yumkini hali ya mambo isiende kulingana na matakwa yake, kwa hiyo sasa amefikia hitimisho kwamba njia ya uhakika ni kuchukua madaraka tena.

Kwa upande mwingine, wapinzani wa Putin ndani ya Russia ambao wana mielekeo ya Kimagharibi, wamekosoa vikali kuendelea kiti cha urais kukaliwa na Putin ambapo sambamba na kumtuhumu kuwa anaunga mkono sera ya kuhodhi utawala wa kisiasa na kifedha wa walio wachache, wanataka mabadiliko na mzunguko wa wasomi, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa ushindani wa kweli katika uga wa uchaguzi wa rais.

 

Pamoja na hayo na kutokana na himaya na uungaji mkono wa Magharibi kwa wapinzani wa Russia hususan Alexei Navalny, kivitendo hawana nafasi kubwa miongoni mwa wananchi wa Russia. Aidha, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni Putin angali juu kileleni kutokana na kuwa na himaya na uungaji mkono mkubwa wa umma.

Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni wa Kituo cha Maoni cha Russia, wananchi wa nchi hiyo wangalia wana imani naye. Asilimia 78.5 ya Warusi wanaafikiana na hatua alizochukua.

Hapana shaka kuwa, Putin akiwa Rais wa Russia amekuwa na jukumu muhimu sana katika maendeleo ya nchi hii katika miongo miwili iliyopita, na ikiwa atashinda uchaguzi ujao wa rais na kuendelea kutawala hadi 2036, inatarajiwa kwamba ataendelea na jukumu lake kuu katika nchi kubwa zaidi ulimwenguni.

Kwa kuzingatia kuendelea kwa vita kati ya Russia na Ukraine na vikwazo vyenye wigo mpana na ambavyo havijawahi kuhuhudiwa vya Magharibi dhidi ya Russia, Putin ameweza kudhibiti matatizo ya Russia kwa kiasi kikubwa. Licha ya ukweli kwamba Russia inakabiliwa na matatizo yanayosababishwa na uhaba wa nguvukazi, mfumuko wa bei na viwango vya juu vya riba,  lakini mafanikio ya Moscow katika kutosalimu amri mbele ya bei mafuta iliyowekwa na Magharibi kwa mafuta ya Russia, na kupanuka mahusiano ya kiuchumi na biashara ya nchi hiyo na  uhusiano na Mashariki ni mambo ambayo yamepelekea kupatikana uthabiti na utulivu wa hali ya uchumi sambamba na kuboreka uchumi wa nchi nchi hiyo

Tags