Utafiti: Aghalabu ya Wamarekani wanapinga Israel kupewa misaada ya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i106306-utafiti_aghalabu_ya_wamarekani_wanapinga_israel_kupewa_misaada_ya_kijeshi
Uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Marekani unaonyesha kuwa, akthari ya wapiga kura nchini humo wanapinga mpango wowote wa Washington kuutumia utawala haramu wa Israel misaada zaidi ya kijeshi.
(last modified 2023-12-22T22:58:13+00:00 )
Dec 22, 2023 22:58 UTC
  • Utafiti: Aghalabu ya Wamarekani wanapinga Israel kupewa misaada ya kijeshi

Uchunguzi wa maoni uliofanyika nchini Marekani unaonyesha kuwa, akthari ya wapiga kura nchini humo wanapinga mpango wowote wa Washington kuutumia utawala haramu wa Israel misaada zaidi ya kijeshi.

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac yanaonesha kuwa, asilimia 46 ya wapiga kura nchini Marekani wanapinga kupewa Israel misaada ya kijeshi na serikali ya Washington.

Asilimia 58 ya wapiga kura wa chama cha Democratic wanapinga kupewa Israel misaada zaidi ya kijeshi kwa ajili ya kuitumia katika vita dhidi ya Ukanda wa Gaza, huku asilimia 65 ya wafuasi wa chama cha Republican wakiunga mkono misaada hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Quinnipiac kwa kuwashirikisha wapigakura 1,647, watu wenye miaka kati ya 18-49 ndio wanaopinga vikali kupewa Israel misaada zaidi ya kijeshi na Marekani. 

Aidha utafiti huo umefichua kuwa, asilimia 59 ya wapiga kura nchini Marekani wanapinga namna Rais Joe Biden anaendesha na kusimamia sera za nje za nchi hiyo.

Rais Biden (kushoto) na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel

Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa hivi karibuni na New York Times na Chuo cha Sinai unaonyesha kuwa, zaidi ya nusu ya wapiga kura wa Marekani (57%) hawakubaliani na sera za Biden kuhusu vita vya Gaza.

Upinzani dhidi ya himaya na misaada ya Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza hauhusiani na wananchi wa Marekani pekee, bali katika nchi nyingine nyingi, watu wanaendelea kuonyesha hasira na kuchukizwa kwao na jinai hizo kwa kufanya mamia ya mikutano na maandamano. 

Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, misaada na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ndio sababu kuu ya kuendelea jinai na mashambulizi dhidi ya wananchi wa Palestina ambayo mpaka sasa yameua Wapalestina zaidi ya 20,000.