WHO: Dunia ichukue hatua za dharura kuzuia maafa zaidi Gaza
(last modified Thu, 28 Dec 2023 06:39:04 GMT )
Dec 28, 2023 06:39 UTC
  • WHO: Dunia ichukue hatua za dharura kuzuia maafa zaidi Gaza

Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mara nyingine tena limeeleza wasi wasi wake kuhusu hali ya kutisha ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua za dharura za kukomesha 'maafa ya kibinadamu' yanayowakabili Wapalestina wa ukanda huo.

Richard Peeperkorn, Mwakilishi wa WHO katika maeneo ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan amesema, "Gaza haifai kuendelea kupoteza hospitali zaidi."

Amesema hospitali 21 hazifanyi kazi kabisa katika Ukanda wa Gaza, na kwamba 2 pekee ndizo zinazofanya kazi kwa kiwango cha chini, huku 13 zikitoa huduma kwa kiwango cha wastani.

Richard Peeperkorn ameeleza bayana kuwa,"Shirika la Afya Dunia linafanya jitihada za kuimarisha na kupanua mfumo wa afya unaofanya kazi kwa sasa Gaza."

Afisa huyo wa WHO amesema makumi ya maelfu ya Wapalestina wanaendelea kuyakimbia maeneo ya katikati mwa Gaza na mji wa Khan Younis wakihofiwa kuuawa na mabomu ya utawala wa Kizayuni.

Maafa ya kibinadamu Gaza

Naye Mratibu wa timu za matibabu ya dharura wa WHO, Sean Casey, ambaye karibuni alizitembelea hospitali kadhaa katikati mwa Gaza amesema, damu zimetapakaa kila mahali katika hospitali za eneo hilo na kwamba alichokiona huko ni mito ya damu na chinjachija ya binadamu" akisisitiza kwamba hakuna mahali salama katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa, takriban huduma zote za afya zimesimama, ama kwa sababu ya kuharibiwa vifaa, au kwa sababu wafanyikazi wamelazimika kukimbia, au kwa dawa zimekwisha na kadhalika.

Zaidi ya Wapalestina elfu 21 wameuawa shahidi wengi wao wakiwa watoto na wanawake, katika mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7 hadi sasa.