Hujuma dhidi ya Waislamu, misikiti Ujerumani zimeongezeka tokea Oktoba 7
Hisia za chuki dhidi ya Uislamu, Waislamu na matukufu yao zimeripotiwa kuongezeka kwa kiwango cha kutisha nchini Ujerumani, tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha mashambulio yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka uliopita 2023.
Shirika la habari la Anadolu limenukuu taarifa ya jumuiya ya Turkish-Islamic Union (DITIB) ambayo imeeleza kuwa, idadi ya barua na nyaraka za chuki na vitisho zinazotumwa misikitini katika nchi hiyo ya Ulaya imeongezeka mno tokea Oktoba 7.
Asasi hiyo ya kiraia yenye makao yake makuu mjini Cologne, kaskazini mwa Ujerumani imesema ina wasi wasi juu ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Waislamu nchini humo kufuatia vita vya utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Kwa mujibu wa Umoja wa Waislamu wa Kituruki nchini Ujerumani (DITIB), Msikiti wa Jamia wa Cologne pekee umepokea barua na baruapepe 17 za vitisho tangu Oktoba 7.
Aidha taasisi hiyo ya kijamii imesema Msikiti wa Selimiye wa jumuiya ya DITIB ulioko katika mji wa kaskazini wa Dinslaken hivi karibuni ulilengwa kwa hujuma hizo za chuki dhidi ya Waislamu na matukufu yao nchini Ujerumani.
Haya yanajiri siku chache baada ya Aiman Mazyek, Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani kusema kuwa, jamii ya Waislamu katika nchi hiyo ya Ulaya inakabiliwa na mashambulizi zaidi dhidi ya misikiti na watu binafsi tokea Oktoba 7 mwaka uliopita, kuliko huko nyuma.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni, Maripota wa Umoja wa Mataifa walieleza kughadhibishwa na kitendo cha serikali ya Ujerumani cha kuunga mkono mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, sambamba na kupinga mashtaka kuhusu mauaji hayo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Hata hivyo wananchi wa Ujerumani wamefanya maandamano mara kadhaa ya kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dharura za kusimamisha mashambulizi hayo ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina, yaliyopelekea kuuawa shahidi Wapalestina zaidi ya 24,000 katika Ukanda wa Gaza,