Ripoti ya Amnesty: Inayamkinika Israel imefanya uhalifu wa kivita Rafah
Amnesty International ya Uingereza imefichua ushahidi wa "mashambulizi yasiyokubalika kisheria" ya mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel katika mji wa Rafah, Gaza, na kueleza kwamba jeshi la utawala huo limetenda uhalifu wa kivita na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu wakati wa mashambulizi ya kikatili katika eneo hilo.
Ripoti iliyotolewa na Amnesty ambayo inachunguza matukio halisi imesema familia nzima zimeteketezwa bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote, na hivyo kuibua wingu zito la shaka juu ya kuwepo maeneo yanayodhaniwa na kudaiwa kuwa "salama" zaidi katika Ukanda wa Gaza.
Uchunguzi uliofanywa na Amnesty International umefuatilia mashambulizi manne tofauti yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni huko Rafah, ambako raia, wakiwemo watoto na wazee, wanaandamwa na mashambulio makubwa ya kikatili.
Mashambulio matatu kati ya hayo yalitokea mwezi Desemba kufuatia kumalizika kwa usitishaji vita kwa ajili ya misaada ya kibinadamu, na jingine lilifanyika Januari.
Erika Guevara-Rosas, mkurugenzi mkuu wa utafiti, utetezi, sera na kampeni katika Amnesty International, amelaani ukatili huo, akiyashutumu majeshi ya Israel kwa kutozingatia sheria za kimataifa na kuharibu maisha ya raia wasio na hatia.
"Familia zote ziliangamizwa katika mashambulizi ya Israel hata baada ya kutafuta kimbilio katika maeneo yaliyotangazwa kuwa salama na bila kutolewa onyo kabla kutoka kwa mamlaka ya Israel," ameeleza afisa huyo wa Amnesty.
Guevara-Rosas amesisitiza kuwa mashambulio hayo yanatilia nguvu ukweli kuhusu mwenendo wa vikosi vya utawala wa Kizayuni vinavyovunja sheria za kimataifa, kinyume na madai ya mamlaka za utawala huo kwamba eti wanachukua hadhari ili kupunguza madhara ya raia.
"Miongoni mwa waliouawa katika mashambulio haya haramu ni pamoja na mtoto wa kike ambaye alikuwa bado hajatimiza wiki tatu, daktari mashuhuri mstaafu mwenye umri wa miaka 69, mwandishi wa habari ambaye alikaribisha nyumbani kwake familia zilizohamishwa, na mama aliyekuwa amelala kitandani na binti yake mwenye umri wa miaka 23", amebainisha afisa huyo wa Amnesty.
Kutolewa kwa ripoti hiyo kumekuja baada ya uamuzi wa muda wa mwezi uliopita wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo iliangazia uwezekano wa mashambulio ya kinyama yanayofanywa na utawala wa Kizayuni katika eneo la Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari…/