Feb 23, 2024 03:30 UTC
  • Kremlin: Biden ameifedhehesha Marekani kwa kumtusi Putin

Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Russia (Kremlin) amesema Rais Joe Biden wa Marekani amelifedhehesha taifa lake analoliongoza kwa hatua yake ya kumtukana hadharani Rais Vladimir Putin wa Russia.

Dmitry Peskov alisema hayo jana Alkhamisi na kueleza kuwa, ni aibu isiyo na kifani kwa rais wa nchi kutoa matusi ya nguoni kadamnasi ya watu dhidi ya rais mwenzake.

"Hii ni fedhehe kubwa kwa Marekani na Wamarekani. Iwapo rais wa nchi anatumia lugha ya aina hiyo, hilo ni jambo la aibu," ameeleza Msemaji wa Ikulu ya Kremlin.

Peskov amesema Biden alitumia lugha hiyo ya kufedhehesha kwa kuiga waigizaji wa Hollywood, akiwa na lengo la kuifurahisha hadhira yake, na kwamba matusi ya namna hiyo kamwe hayawezi kumuumiza kiongozi wa nchi yoyote ile, achilia mbali Rais Putin.

Biden siku ya Jumatano akihutubia mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kampeni zake za kuwania urais kwa muhula wa pili huko San Francisco, alitoa matusi ysiyoelezeka dhidi ya Putin akidai kuwa rais huyo wa Russia ni chakaramu.

Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Russia (Kremlin), Dmitry Peskov

Hii si mara ya kwanza kwa Biden kuwatukana viongozi wa Russia na hata wa nchi waitifaki wa Washington. Wiki iliyopita, vyombo vya habari viliripoti kuwa, rais huyo mkongwe wa Marekani alitoa matusi ya nguoni mara kadhaa dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Uhusiano wa Russia na Marekani uliharibika zaidi baada ya kuanza kwa vita vya Ukraine. Nchi za Ulaya na Marekani zinaendelea kuiunga mkono kikamilifu Ukraine kwa silaha na mali dhidi ya Russia, na hivi karibuni serikali ya Washington ilitangaza msaada mwingine wa kijeshi wenye thamani ya mamilioni ya dola.

 

Tags