ICJ kuanza kusikiliza kesi ya mauaji ya kimbari inayoikabili Ujerumani Aprili
(last modified Sat, 16 Mar 2024 07:21:51 GMT )
Mar 16, 2024 07:21 UTC
  • ICJ kuanza kusikiliza kesi ya mauaji ya kimbari inayoikabili Ujerumani Aprili

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ wamesema kesi iliyowasilishwa na Nicagarua ikiishtaki Ujerumani kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina itaanza kusikilizwa mwezi ujao wa Aprili.

Taarifa ya jana Ijumaa ya mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imesema, majaji wa korti hiyo ya kimataifa watafanya vikao vya kusikiliza pande zote kwenye kesi hiyo dhidi ya Ujerumani Aprili 8 na 9.

Wiki mbili zilizopita, Nicaragua ilizishitaki Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Canada katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji yake ya kimbari ya Wapalestina.

Serikali ya Managua ilitangaza katika taarifa rasmi kwamba, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na Canada zinahusika katika ukiukaji mkubwa na wa kimpangilio wa Mkataba wa Kuzuia na Kutoa Adhabu kwa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari na Sheria za Kimataifa za Masuala ya Kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na serikali ya Nicaragua, nchi nne za Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Canada zimetakiwa pia ziache kupeleka silaha, risasi na teknolojia za kijeshi kwa utawala wa Kizayuni.

Mauaji ya kimbari Gaza

Kwa mujibu wa Nicaragua, kwa vile ICJ iliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza katika hukumu yake ya Januari 26, Israel inapaswa kuhakikisha inachukua hatua zinazohitajika ili kuzuia kuendelea mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Katika hatua nadra kushuhudiwa na katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 2024, serikali ya Afrika Kusini iliwasilisha mashtaka dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikiutuhumu utawala huo wa Kizayuni kwamba unafanya jinai ya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Wapalestina karibu 32,000, wengi wao wakiwa watoto, wanawake na wazee wameuawa shahidi tangu ulipoanza uvamizi na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.