Wananchi wa Uturuki washiriki katika uchaguzi muhimu wa serikali za mitaa
Vituo vya kupigia kura nchini Uturuki vilifunguliwa mapema leo asubuhi kuruhusu wananchi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotajwa kuwa ni mtihani muhimu kwa Rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi hiyo. Weledi wa mambo wanasema kuwa Rais wa Uturuki anakabiliwa na kibarua kigumu ili kuyarejesha maeneo muhimu ya mijini aliyoshindwa na upinzani miaka mitano iliyopita.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi leo Jumapili kwa saa za Uturuki huku upigaji kura ukianza saa mbili asubuhi katika maeneo mengine na kumalizika saa kumi na moja jioni.
Uchaguzi wa leo wa serikali za mitaa nchini Uturuki unatajwa kuwa kipimo kitachoweka wazi kiwango cha ushawishi na uungaji mkono wa wananchi kwa Erdogan; uchaguzi ambao utaonyesha ni chama kipi kinastahiki kupata viti vingi na hivyo kuuongoza mji wa Istanbul ambao ni kitovu cha uchumi wa nchi hiyo, na mji mkuu wa Ankara, ambao Erdogan na chama chake tawala cha Kiislamu cha Haki na Maendeleo waliupoteza kwa wapinzani mwaka 2019.
Rais Recep Erdogan aliye na umri wa miaka 70 ameahidi kuikomboa Istanbul, mji wenye jamii ya watu milioni 16 alikozaliwa na kukulia; sehemu ambayo pia alianzia shughuli zake za kisiasa akiwa Meya wa mji huo mwaka 1994.
Evren Balta Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Ozyegin cha Uturuki anasema: "Kushinda miji mikubwa ni nuhinu zaidi kwa upinzani, lakini pia inamaanisha kupata pesa za kigeni, kuwa na uhusiano wa kimataifa na wadau wa uchumi na wahusika wa kisiasa."