Apr 01, 2024 10:43 UTC
  • Shambulizi la Moscow... Russia yaitaka Kiev kumkabidhi mkuu wa usalama

Russia imeitaka Ukraine kuwakabidhi raia wake kadhaa, akiwemo Mkuu wa Idara ya Usalama ya nchi hiyo, kwa madai kwamba walihusika na vitendo vya "kigaidi" katika ardhi ya Russia, suala ambalo Kiev imelitaja kuwa takwa"lisilo na thamani".

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imekariri, katika taarifa yake, kwamba Ukraine ina uhusiano na shambulio la umwagaji damu lililotokea tarehe 22 mwezi huu kwenye ukumbi wa tamasha karibu na Moscow.

Kamati ya Uchunguzi ya Russia ilithibitisha - Alhamisi iliyopita - kwamba wahusika wa shambulio dhidi ya  ukumbi wa tamasha wa Crocus City Hall nje kidogo ya jiji la Moscow walikuwa na "mahusiano na wanaharakati wa Kiukreni" na walipokea pesa nyingi kutoka Ukraine.

Russia pia imetilia shaka madai ya Marekani kwamba kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limehusika na shambulio hilo ambalo liliua watu 137, linalotajwa kuwa la umwagaji damu mkubwa zaidi ndani ya Russia katika miongo miwili. 

Mmoja wa watuhumiwa wa shambulio la Crocus City Hall

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema kwamba, kwa kuzingatia mikataba miwili ya kimataifa ya kupambana na ugaidi, imeitaka Ukraine "kuwakamata mara moja na kuwakabidhi" watu kadhaa, akiwemo Mkuu wa Idara ya Usalama, Vasyl Maliuk.

Imeongeza kuwa Malyuk alikiri "kupanga mlipuko wa Daraja la Crimea mnamo Oktoba 2022 na kufichua maelezo ya kuandaa mashambulio mengine ya kigaidi."

Siku kadhaa zilizopita, Rais wa Russia, Vladimir Putin alisema kuwa watu 11 wamekamatwa, wakiwemo wanne waliokimbia kutoka kwenye ukumbi wa Crocus City Hall na kuelekea eneo la Bryansk, wakiwa na nia ya kuvuka mpaka na kuingia nchini Ukraine.

Tags