Apr 13, 2024 07:26 UTC
  • Ufaransa, India, Russia, Uingereza zaonya raia wao kutokwenda Israel

Nchi kadhaa zikiwemo Ufaransa, India, Russia, Poland na Uingereza zimewaonya raia wao dhidi ya kusafiri kwenda Israel, huku kukiwa na jibu linalotarajiwa la Iran kwa shambulio la kigaidi la utawala wa Israel kwenye ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria mapema mwezi huu.

Katika hotuba yake mjini Tehran siku ya Jumatano, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alisema utawala wa Israel "lazima uadhibiwe na utaadhibiwa" kwa shambulio lake dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran mnamo tarehe Aprili 1.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa siku ya Ijumaa iliwashauri raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Israel, Lebanon,  Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Gaza.

Uingereza iliwaambia raia wake waepuke safari zote isipokuwa muhimu kuelekea Israel na Palestina kutokana na "uwezekano wa Iran kuishambulia Israel."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilionya dhidi ya "safari zote" kwenda kaskazini mwa Israel, Ukanda wa Gaza, maeneo ya karibu na Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa jwa mabavu.

Makombora ya Iran yameutia kiwewe utawala wa Kizayuni wa Israel

Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Poland pia imeshauri dhidi ya kusafiri kwenda Israel, Palestina na Lebanon. India nayo pia imewataka raia wake kutosafiri Israel.

Wakati huo huo, jeshi la Israel lilitoa taarifa siku ya Ijumaa ambapo lilionya kwamba siku zijazo vikosi vyake vinapaswa "kuwa macho na kujiandaa."

Haya yanajiri wakati Iran imeapa kuiadhibu Israel kwa shambulizi la anga la Aprili 1 kwenye ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus.

Shambulizi hilo la Israel liliwaua wanajeshi wawili waandamizi wa jeshi la Iran waliokuwa washauri wa kijeshi nchini Syria pamoja na maafisa watano walioandamana nao.