May 04, 2024 06:56 UTC
  • Vladimir Putin
    Vladimir Putin

Ofisi ya Rais wa Russia jana Ijumaa ilishutumu kauli zilizotolewa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kuhusu uwezekano wa Paris kuingia katika vita vya Ukraine, na kuzitaja kuwa ni "mwenendo hatari sana."

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba: "Taarifa hii ni muhimu sana na hatari sana," na kuongeza kwamba Macron "anaendelea kuzungumzia uwezekano wa kuingia moja kwa moja katika vita wa Ukraine."

Haya yanajiri baada ya Macron kukariri - wakati wa mahojiano yaliyochapishwa na jarida la Uingereza la The Economist, Alhamisi iliyopita- nia yake ya kutuma vikosi vya jeshi la Ufaransa nchini Ukraine, iwapo Moscow itavuka "mstari wa mbele" na ikiwa Ukraine itawasilisha maombi katika suala hili.

Jarida hilo lilisema kuwa matamshi ya Macron yamekuja baada ya tangazo lake wiki iliyopita kwamba "Ulaya inaweza kusambaratika kwa kiasi" kutokana na mvutano unaoongezeka unaotokana na vita vya Russia na Ukraine.

Hii si mara ya kwanza kwa rais wa Ufaransa kuzungumzia chaguo hili, kwani mwezi uliopita wa Machi aliibua suala la kutuma vikosi vya majeshi ya nchi za Magharibi huko Ukraine, jambo ambalo lilizua mzozo miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO).

Moscow ilijibu pendekezo la Ufaransa kupitia mkurugenzi wa Huduma ya Ujasusi wa Kigeni wa Russia, Sergei Naryshkin, ambaye alitishia kwamba iwapo Paris itatuma jeshi huko Ukraine, "litakuwa shabaha halali ya vikosi vya jeshi la Russia."